Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na Waziri wa Uchumi na Biashara za kimataifa wa Ufaransa Mhe. Franck Riester, Ikulu Jijini Dar es salaam. Oktoba 19,2021
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akimkabidhi zawadi ya Kinyago cha Umoja Waziri wa Uchumi na Biashara za kimataifa wa Ufaransa Mhe. Franck Riester mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao Ikulu Jijini Dar es Salaam. Oktoba 19,2021
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Uchumi na Biashara za kimataifa wa Ufaransa Mhe. Franck Riester,(Kulia) Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Mabalozi kutoka Tanzania na Ufaransa , Ikulu Jijini Dar es salaam. Oktoba 19,2021.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo Oktoba 19,2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Uchumi na Biashara za kimataifa wa Ufaransa Mhe. Franck Riester, Ikulu Jijini Dar es salaam.
Katika Mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine Waziri Riester ameleta salamu maalum pamoja na mwaliko Rasmi wa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. Waziri Riester amesema Ufaransa inatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania ikiwemo kuboresha mazingira ya biashara pamoja na kuleta usawa wa kijinsia mambo ambayo pia yanatiliwa mkazo na serikali ya Ufaransa.
Amesema Ufaransa imedhamiria kuongeza ushirikiano na Tanzania kwa manufaa ya nchi zote mbili huku akitoa mfano wa kuanzishwa kwa usafiri wa ndege wa moja kwa moja kutoka Paris Nchini Ufaransa hadi Zanzibar ulioanza hivi karibuni ambao ulisimama kwa miaka 47. Waziri huyo wa Uchumi wa Ufaransa ameambatana na Wafanyabiashara mbalimbali kutoka Ufaransa wenye nia ya kuwekeza nchini
Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango amewakaribisha wawekezaji kutoka Nchini Ufaransa na kuwahakikishia Tanzania ni Nchi salama kuwekeza iliojaariwa rasilimali nyingi na fursa lukuki. Amesema pamoja na changamoto za kiuchumi zilizosababishwa na Uviko 19, serikali imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali kupambana na hali hiyo ikiwemo kutoa chanjo ili kukabiliana na ugonjwa huo.
Aidha amesema Ufaransa imekua kati ya wadau wakubwa wa maendeleo nchini Tanzania na uwekezaji katika sekta mbalimbali hapa nchini ikiwemo ujenzi wa Miundombinu , Elimu pamoja na Maji huku akiwakaribisha kuwekeza katika sekta ya Afya hususani ujenzi wa viwanda vya dawa, sekta ya Utalii na Nishati.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Mawaziri kutoka serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar , Balozi wa Tanzania Nchini Ufaransa pamoja na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments: