Naibu kamishna wa Uhifadhi wa NCAA (Huduma za Shirika) Needpeace Wambuya (kushoto) akizungumza na Maafisa Wanafunzi kutoa chuo cha Kijeshi Monduli Mkoani Arusha (hawapo pichani) walipotembelea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, kushoto kwa Naibu Kamishna ni Mshauri wa masuala ya kieshi wa NCAA Kanali Henry Komba.
Kaimu kamishna Msaidizi Mwandamizi (Huduma za Utalii) Peter Makutian akizungumza na Maafisa wanafunzi wa chuo cha Kijeshi Monduli wakati wa ziara yao katika eneo la Hifadhi la Ngorongoro tarehe 20 oktoba, 2021.
Maafisa wanafunzi kutoka chuo cha kijeshi Monduli wakisilikiza maelezo kuhusu historia ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro pamoja ya shughuli za utalii na uhifadhi zinazofanyika katika eneo hilo.
Mshauri wa masuala ya Kijeshi wa NCAA Kanali Henry Komba (wa pili kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na maafisa wanafunzi kutoka chuo cha Kijeshi Tanznaia kilichopo Monduli mkoani Arusha.
Na Kassim Nyaki-NCAA
Maafisa wanafunzi 84 kutoka chuo cha Kijeshi (Tanzania Millitary Academy) kilichopo Monduli Mkoani Arusha leo tarehe 20 oktoba, 2021 wametembelea eneo la hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kujifunza shughuli mbalimbali za uhifadhi na kujionea vivutio vya utalii vinavyopatikana katika eneo hilo.
Kiongozi wa Maafisa wanafunzi hao Meja Said Chombo ameibainisha kuwa pamoja na wanafunzi hao kusoma mambo ya kijeshi wameona kuna umuhimu wa kuwatembeza katika maeneo ya Hifadhi ili kujifunza mambo ya Uhifadhi, utunzaji wa mazingira, utalii na shughuli za maendeleo ya jamii.
“Wanajenshi ni sehemu ya Jamii, na sisi kama wazalendo katika nchi yetu tunaona umuhimu wa kutembelea na kuona rasilimali tulizonazo katika nchi yetu ili kuwa mabalozi wa kutangaza vivutio vya utalii lakini pia kutoa elimu kwa jamii zetu kuona umuhimu wa kutunza mazingira hasa yaliyohifadhiwa” aliongeza Meja Chombo.
Akipokea ujumbe wa maafisa hao Naibu Kamishna wa NCAA (Huduma za Shirika) Bw. Needpeace Wambuya amebainisha kuwa NCAA itaendelea kudumisha uhusiano na vyombo vya Ulinzi na usalama kama jeshi la Wananchi wa Tanzania ambao wamekuwa wakitembelea Hifadhi ya Ngorongoro mara kwa mara kwa shughuli za utalii na kujifunza mambo mbalimbali ya kiuhifadhi.
Kaimu kamishna Msaidizi mwandamizi wa NCAA anayesimamia huduma za Utalii Peter Makutian ameeleza kuwa eneo la hifadhi ya Ngorongoro ni la kipekee ambapo wageni wanaweza kuona vitu vingi kwa wakati mmoja ikiwemo Wanyamapori wa aina mbalimbali, chimbuko la binadamu wa kale duniani, kreta ya Ngorongoro, Uhifadhi wa misitu na mazingira pamoja na utalii wa kitamaduni kwa jamii zinazoishi ndani ya hifadhi hiyo.
Wakiwa katika eneo la Hifadhi hiyo maafisa hao kutoka chuo cha Kijeshi Monduli walifanikiwa kutembelea eneo la kreta ya Ngorongoro, makumbusho ya Olduvai pamoja na kushuhudia uhifadhi wa msitu wa Nyanda za juu kaskazini ambao ni makazi ya wanyama kama tembo, Nyati, faru, chui na wengineo, msitu huo pia ni chanzo kikubwa cha maji kwa wananchi wanaozunguka hifadhi ya Ngorongoro hasa vijiji vya Karatu na Monduli mkoani Arusha.
Toa Maoni Yako:
0 comments: