SALAAM ZA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO MHE. DKT. DOROTHY.O GWAJIMA KUELEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI TAREHE 08/03/2021 INAYOFANYIKA KIMKOA NCHINI TANZANIA.

Napenda kuwapongeza na kuwatia moyo wanawake wote nchini Tanzania kwa nafasi yao kama wanawake kwenye kuchangia maendeleo ya taifa hili ngazi zote. Nawapongeza kwa Kauli Mbiu nzuri ya siku hii ya “Wanawake katika Uongozi; Chachu Kufikia Dunia yenye Usawa.

Nawahakikishia kuwa Serikali ya Tanzania inajali wanawake na iko mstari wa mbele kutekeleza mipango endelevu ya maendeleo yenye nguzo za kisheria na kisera. Kwa mfano;
1. Serikali inatekeleza mpango wa kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia mikopo ambapo kwa mwaka 2019/2020 imetoa mikopo ya thamani ya Tsh Bilioni 23.8 iliyonufaisha Vikundi 6859 vya Wanawake Wajasiriamali.

2. Serikali inatekeleza mpango wa kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake (MTAKUWWA) ambapo kuna Kamati rasmi hadi ngazi ya Jamii, Wilaya na Mkoa. Kamati hizi zinasimamia, zinaelimisha na kufuatilia vitendo vyote vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na kuchukua hatua stahiki.

3. Kwa upande wa elimu Serikali inajali watoto na sasa inatekeleza sera ya elimu bila malipo kwa watoto wote wa Kitanzania.

4. Serikali haijawaacha nyuma wanawake kwenye nafasi za uongozi ngazi zote kuanzia Mheshimiwa Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu, Mheshimiwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Akson, Waheshimiwa Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na wengine wengi.

5. Kwenye huduma za Afya bajeti karibu 75% inazingatia huduma za afya kwa wanawake wajawazito na watoto.

Hivyo, kwa mifano hii michache napenda kuwahakikisha Wanawake na Watoto kuwa wako salama chini ya Uongozi wa Rais Dkt John Pombe Magufuli ambaye Serikali yake siku zote imeendelea kuzingatia mustakabali wa maendeleo na ustawi wao.

Kwa salaam hizi fupi naomba niwatakie Wanawake wote Sikukuu njema yenye furaha, amani na upendo huku wakikumbuka kuwa „Wanawake katika Uongozi; Chachu Kufikia Dunia yenye Usawa”. Aidha, Wito wangu kwa Wanawake wote ambao tupo kwenye nafasi mbalimbali za uongozi tuzidi kushikamana na kushirikiana kuzingatia kusimamia haki, usawa na maslahi ya wanawake na watoto daima.

Mungu Ibariki Siku ya Wanawake Duniani Tarehe 08/03/2021.

Dkt. Dorothy Gwajima (Mb)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO
07/03/2021
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: