Mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini Justine Monko akizungumza na wananchi wa AMCOS ya Ughandi wanaojishughulisha na kilimo cha pamba muda mfupi kabla ya kumkaribisha Naibu waziri wa Kilimo.
 Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akizungumza na wananchi wa AMCOS ya Ughandi wanaojishughulisha na kilimo cha pamba halmashauri ya wilaya ya Singida vijijini wakati wa ziara yake.
 Meneja wa Uhusiano na Utumishi wa kiwanda cha Mount Meru Singida Bw. Nelson Mwakabuta akisoma taarifa fupi ya kiwanda hicho mbele ya Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba muda mfupi baada ya kutembelea kiwanda hicho wakati wa ziara yake mkoani Singida. 
 Meneja wa Uhusiano na Utumishi wa kiwanda cha Mount Meru Singida Bw. Nelson Mwakabuta akisoma taarifa fupi ya kiwanda hicho mbele ya Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba muda mfupi baada ya kutembelea kiwanda hicho wakati wa ziara yake mkoani Singida.
 Mkurugenzi wa kiwanda cha Singida Fresh Oil Mill, maarufu Kilimo Kwanza, Khalid Ally  Omary akimuonesha Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba (katikati) aina ya mbegu mbalimbali za alizeti zinazofaa kwa uzalishaji bora wa mafuta ya kupikia. Kushoto ni Mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini, aliyemwakilisha mbunge wa Singida Mjini Mussa Sima.   
 Mkurugenzi wa kiwanda cha Singida Fresh Oil Mill, maarufu Kilimo Kwanza, Khalid Ally  Omary akitoa taarifa fupi ya kiwanda hicho mbele ya Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba alipotembelea kiwanda hicho kilichopo katika halmashauri ya wilaya ya Manispaa ya Singida.
 Mkurugenzi wa kiwanda cha Singida Fresh Oil Mill, maarufu Kilimo Kwanza, Khalid Ally  Omary akitoa taarifa fupi ya kiwanda hicho mbele ya Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba alipotembelea kiwanda hicho kilichopo katika halmashauri ya wilaya ya Manispaa ya Singida.
 Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akiangalia sehemu ya uzalishaji unaofanywa na kiwacha cha kukamua alizeti cha Singida Fresh Oil Mill, maarufu Kilimo Kwanza wakati wa ziara yake.


Mkurugenzi wa kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti cha Choice Kindai, Bi. Amina Dang’ati akimuonesha Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba sehemu ya uzalishaji unaofanywa na kiwanda hicho, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi ya Mheshimiwa Mgumba mkoani Singida.
Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba (watatu kutoka kushoto waliosimama) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi na uongozi wa kiwanda hicho. (kushoto waliosimama ni Mbunge wa Singida Kaskazini Justine Monko.

Na Dotto Mwaibale, Singida

WASINDIKAJI wa viwanda vya kuzalisha mafuta ya alizeti nchini wameomba serikali kuzifanyia marekebisho tozo za VAT zilizopo kwenye eneo hilo ili kuongeza tija, kutokana na tozo hiyo kuonekana kikwazo kinachopelekea kufifisha ustawi wa viwanda hivyo na kutoa fursa kwa viwanda vya nje kuchukua nafasi kubwa.

Wakizungumza mbele ya Naibu Waziri wa kilimo, Omary Mgumba, wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi kukagua miradi mbalimbali ya kilimo mkoani hapa, wadau hao wameiomba serikali kuondoa tozo kwenye mnyororo mzima wa uzalishaji wa mafuta hayo na ikiwezekana kutoa ruzuku ya ununuzi wa mbegu bora za alizeti na viuatilifu kwa wakulima ili kuongeza tija na kuwezesha bidhaa hiyo kukidhi mahitaji

“Alizeti ni chache, na wakati wa mavuno tunajikuta hatupo peke yetu tunakabiliwa na ushindani mkubwa wa kupata hiyo alizeti, sisi mashine zetu tumeziminya mpaka kwa siku tukiwa na alizeti nyingi tunaweza kuzalisha tani mia tatu pekee (300) kwa siku wakati uwezo wa mashine zetu ni kuzalisha mpaka tani mia saba na hamsini (750) kwa siku,” alisema Meneja Utumishi na Uhusiano wa Kiwanda cha Mount Meru, Nelson Mwakabuta

 Mwakabuta aliiomba serikali kuwapatia wakulima ruzuku ya mbegu na kuongeza wazalishaji wa mbegu ya alizeti ili kuwezesha mbegu hiyo kupatikana kwa wingi na kwa kuzingatia ubora stahiki kulingana na matakwa ya soko la ndani na nje. Alisema mbegu za kienyeji hutoa uzito mkubwa lakini mafuta ni kidogo ukilinganisha na zile za kisasa

Alisema kuna aina ya mbegu za kienyeji mathalani Jupita chotara kwa gunia moja inatoa uzito wa kilo 75-80, lakini za kisasa hybrid inatoa 60 mpaka 65. Alifafanua kuwa mbegu aina ya Hybrid dukani inauzwa kwa sh. 7000 kwa kilo, huku akisisitiza kuwa kuna mbegu bora iliingia mwaka uliopita nchini ijulikanayo kama ‘Hisen 33’ yenye sifa ya kuvumilia ukame na hata ikiwa kwenye mvua nyingi haiharibiki inauzwa sh 35,000, ukimwambia mkulima anunue mbegu hiyo hawezi kumudu mpaka awezeshwe

Alisema anaomba serikali ilegeze masharti ya kuingiza mbegu za kigeni nchini ikiwezekana zije kwa wingi, tofauti na mchakato wake kwa sasa ambao hadi kukamilisha taratibu zote za uingizaji na hatimaye kuingia sokoni huchukua kati ya miaka 5 hadi 6

Aidha, mwakilishi huyo wa Mt Meru alisema kumekuwepo na ushindani wa soko usio wa haki kwa baadhi ya wasindikaji wadogo ambao hata hawalipi kodi yoyote ya uzalishaji kuuza mafuta ya alizeti zaidi ya kiwango stahiki, mathalani mtu anaponunua lita 20 huongezewa na lita 5 zaidi hali inayoondoa usawa na ushindani wa biashara hiyo sokoni na kupelekea kuua viwanda ambavyo vipo kwenye mfumo wa ulipaji kodi

Mwakabuta alisema, viwanda vikubwa kikiwepo Mt Meru wamekuwa wakinunua mashudu kutoka kwenye viwanda vidogo lakini kinachoumiza ni pale wanapopita magetini au kwenye vizuizi vya barabara hulazimika kutozwa tozo ya ushuru wa mashudu hayo na halmashauri kufikia hadi sh elfu 20 kwa tani

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Mafuta ya Alizeti cha Singida Fresh Oil Mill maarufu “Kilimo Kwanza,” Khalid Ally Omary aliiomba serikali kuondoa tozo kwenye tasnia nzima ya mnyororo wa uzalishaji wa mafuta hayo kwa wasindikaji wa ndani ili kuleta ushindani wa kibiashara kwa waingizaji wa nje lakini pia kukidhi hitaji la soko

Alisema wanajitahidi sana kwenda na kasi ya serikali ya Awamu ya Tano ya uchumi wa viwanda lakini wanakwamishwa na tozo mbalimbali ndani ya serikali na halmashauri, huku akiomba wapatiwe ‘exemption’ japo ya mda kuweza kuingiza vifaa na vipuri muhimu vya kustawisha viwanda vyao kwa masharti ya kulipa kwa utaratibu maalumu

“Alisema Fresh Oil Mill wana kiwanda kikubwa cha mafuta ya alizeti hapa Singida ambacho kimekwama kwa takribani miaka mitatu sasa kutokana na kukosa msamaha au punguzo lolote la kodi kuweza kusaidia uingizaji wa vipuri na vifaa vingine kukiwezesha kuanza rasmi kufanya kazi

Alisema kwa sasa wana kiwanda cha kati kinachozalisha tani 720 kwa mwezi huku kikifanikiwa kutoa  ajira za watu 167 lakini wanakabiliwa na tozo kubwa ya VAT kwenye uzalishaji mzima wa mnyororo wa bidhaa hiyo kiasi cha kupelekea bei ya mafuta hayo kupanda na kushindwa kuhimili ushindani wa mafuta yanaoingizwa toka nje ambayo huuzwa kwa gharama ndogo

Changamoto nyingine ya uzalishaji wa bidhaa hiyo ni kukosa ubora wa mbegu za alizeti zinazokidhi viwango. Omary alisema mbegu nyingi zinazozalishwa zina uzito lakini zikikamuliwa hazina mafuta ya kutosha

Aidha, alimweleza Naibu Waziri wa Kilimo kuwa tatizo lingine linayoikumba sekta hiyo ni msururu wa kodi kwenye eneo la vipimo na uhakiki wa bidhaa hiyo ambayo hutozwa hadi sh laki moja kwa kila ‘item’ moja. Mathalani Kodi ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi  inatozwa na taasisi mbili yaani OSHA na Manispaa

Akijibu baadhi ya changamoto hizo, Naibu Waziri Mgumba alisema kero nyingi zilizowasiliswa ni mtambuka ambazo zinagusa zaidi ya wizara moja, hivyo kwa kuzingatia usikivu wa serikali ya awamu ya tano na kauli mbiu iliyopo ya Tanzania ya Viwanda atakaa na viongozi wenzake kuangalia namna nzuri ya kurekebisha ili kuongeza tija kwenye sekta hiyo

Akizungumzia hoja ya uhaba wa mbegu, alisema serikali imewawezesha ASA kuzalisha mbegu za kutosheleza mahitaji na zenye ubora stahiki kulingana na mahitaji ya soko. Aliwashauri wasindikaji kuingia mikataba na wakulima kwa kuwakopesha mbegu na kisha kulipana baada ya mavuno

Mgumba alisema mwarobaini pekee wa kukabiliana na ushindani wa mafuta yanayoingizwa nchini ni kwa wasindikaji wa sekta hiyo kuzalisha kwa wingi bidhaa hiyo na kutosheleza mahitaji ya nchi nzima

“Serikali wala haina tatizo mkizalisha kwa wingi kiwango cha kutosheleza mahitaji ya nchi sisi tutazuia tu mafuta toka nje yasiingie au tutapandisha kodi kwa asilimia mia moja,” alisema Mgumba huku akiwahimiza wasindikaji hao kuzidisha uzalishaji sanjari na wale wenye mitaji inayosuasua kuitumia Benki ya Kilimo ya TIB

Aidha, pamoja na mambo mengine alimtaka Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida kuitisha kikao kitakachowakutanisha wasindikaji wote wa viwanda vikubwa na vya kati, wakulima na mabenki kujadili kwa kina changamoto zilizopo, ikiwemo kuangalia namna bora kunyanyua uzalishaji wa mafuta ya alizeti

Aidha, katika ziara hiyo, Mgumba akiongozana na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Singida alipata fursa ya kutembelea na kujionea hali halisi ya kilimo na uzalishaji kwenye vijiji na Kata mbalimbali ndani ya Singida DC, ikiwemo viwanda vikubwa na vya kati vya kukamua mafuta ya alizeti.

Maeneo mengine aliyotembelea ni bonde la kilimo la Ntambuko, skimu ya umwagiliaji ya Kata ya Msange, na baadaye alikutana na kufanya mkutano na wakulima wa pamba kupitia AMCOS ya Ughandi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: