Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi ya Zanzibar, Mheshimiwa Assaa Ahmad Rashid akiongea katika kikao kifupi baina yake na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu walipokutana mapema leo Novemba 28, 2019 katika hoteli ya Madina Al Bahr iliyopo Visiwani Zanzibar. Kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu na Wa kwanza kulia ni Mwakilishi kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo, Paul Turay.
Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi ya Zanzibar, Mheshimiwa Assaa Ahmad Rashid akiongozana kuelekea katika chumba cha mkutano na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu Novemba 28, 2019 katika hoteli ya Madina Al Bahr iliyopo Visiwani Zanzibar.
Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi ya Zanzibar, Mheshimiwa Assaa Ahmad Rashid akiteta jambo na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu walipokutana mapema leo Novemba 28, 2019 katika hoteli ya Madina Al Bahr iliyopo Visiwani Zanzibar.

NA MBARAKA KAMBONA.

MWENYEKITI wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu ameitaja tasnia ya habari kuwa ndio wadau wakubwa wa haki za binadamu nchini.

Jaji Mwaimu alitoa kauli hiyo Novemba 28, 2019 katika mkutano uliofanyika Visiwani Zanzibar wa kuwajengea uelewa wa pamoja Makamishna wa tume walioteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli.

Jaji Mwaimu alieleza katika mkutano huo kuwa katika kutekeleza jukumu walilopewa la kulinda, kuhifadhi na kutetea haki za binadamu chini wanawategemea sana vyombo vya habari kuelimisha jamii kuhusu haki zao.

“Vyombo vya habari ni wadau wetu wakubwa sana, wao ndio waelimishaji, wao ndio wamekuwa wakati wote wakiibua matukio mbalimbali ya uvunjifu wa haki za binadamu kwa lengo la kuujulisha au kuelimisha umma”,alisema Jaji Mwaimu

“Nyie ndio mtakaoitangaza tume, kwa msingi huo, niseme kuwa tutaendelea kuwashirikisha katika yale yote tutakayokuwa tunayafanya ili kupitia nyinyi wananchi watafahamu kuhusu tume inachokifanya”,aliongeza

Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa tume haiwezi kufanya kazi peke yake bila kushirikiana na wadau wengine kama vyombo vya habari, Idara nyingine za serikali, Asasi za Kiraia na taasisi za kimataifa.

“Ni lazima tujenge mahusiano mazuri ya kazi baina yetu, hatuwezi kufanya kazi peke yetu, ni muhimu kufanya kazi na idara mbalimbali ikiwemo wadau wa maendeleo”, alisisitiza

Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi ya Zanzibar, Assaa Ahmad Rashid, ambaye ndiye aliyefungua mkutano huo kama mgeni rasmi, alimueleza Jaji Mwaimu kuwa dhamana waliyopewa ni kubwa, kwa kuwa haki za binadamu ndio msingi katika nchi yetu, wameaminiwa hivyo hawana budi kulitekeleza jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa ili kuwasaidia wananchi.

“Jukumu mlilopewa Serikali ni kubwa, sisi tunawaahidi kuwa tutaendelea kutoa ushirikiano katika kuifanya tume iweze kutekeleza majukumu yake vizuri”, alisema Rashid

Rashid aliendelea kusema kuwa Kuteuliwa kwa viongozi hao kunatoa fursa kamili na ya wazi kwa mwananchi kupeleka lalamiko lake, na kwamba serikali imejenga mazingira mazuri ya kufanya kazi kwa wadau wote hususani Asasi za Kiraia, na wakati wote serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zote ikiwemo za kimataifa ili kuhakikisha yale malengo yaliyowekwa yanafikiwa.

“Tunatambua kuwa katika kutekeleza majukumu yenu kuna changamoto mnazo kutana nazo, ikiwemo uelewa mdogo wa wananchi kuhusu haki zao,lakini muendelee kueneza elimu hiyo kwa kushirikiana na taasisi zingine”,aliongeza Rashid.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: