Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Vicente Muanda wakiwa katika ukumbi wa mikutano, mjini Brazzaville jana
Balozi wa Tanzania Nchini DRC Luteni. Jen. Paul Mella akimueleza jambo balozi wa sudan wakati wa mkutano wa ukanda wa maziwa makuu mjini Brazzaville jana
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa ukanda wa maziwa makuu wakifuatilia mkutano ulifanyika jana Brazzaville jana
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro akiwasilisha pendekezo la Kiswahili kutumika katika ukanda wa maziwa makuu mjini Brazzaville jana
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa ukanda wa maziwa makuu wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kongo, Bwn. Clement Mouamba jijini Brazzaville jana
Na Mwandishi wetu, Brazzaville,
Katika jitihada za kukuza lugha ya Kiswahili barani Afrika, Tanzania imeziomba nchi wanachama wa ukanda wa maziwa makuu kuanza kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi na lugha ya kazi
Wito huo umetolewa katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa ukanda wa maziwa makuu, uliofanyika mjini Brazzaville leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro
"Tumewaomba wenzetu wa maziwa makuu wakubali lugha ya Kiswahili kutumika kama lugha rasmi na lugha ya kazi katika nchi zote za maziwa makuu. Pia nchi sita ambazo zipo hapa na hazijaridhia mabadiliko ya mkataba wa Afrika kuruhusu Kiswahili kutumika kama lugha rasmi katika Afrika (AU) nchi hizo zimetuhakikishia kuwa zitaridhia mabadiliko hayo ili kuhakikisha kuwa Kiswahili kinaanza kutumika kama lugha rasmi ya kazi," Alisema Dkt. Ndumbaro
Kwa mujibu wa Waziri Ndumbaro, matumizi ya lugha ya Kiswahili katika ukanda huo ni fursa ambayo italeta umoja wa kitaifa, na katika ukanda wa maziwa makuu lakini pia umuhimu wa Kiswahili kwamba ni lugha pekee ambayo haina uhusiano na ukoloni barani afrika.
"Tunatumaini kwamba tutazipata sahihi za nchi sita na tukisha zipata tutabakiwa na sahihi ya nchi moja tu ili Kiswahili kiwe rasmi lugha ya kazi katika mikutano itakayo kuwa inafanyika barani Afrika," aliongeza Dkt. Ndumbaro
Nchi sita ambazo hazijaridhia mabadiliko ya mkataba wa Afrika kuhakikisha kuwa Kiswahili kinatumika kama lugha rasmi ya kazi ni pamoja na Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudani, Uganda na Zambia.
Kwa sasa hivi ni lugha rasmi lakini siyo lugha ya kazi kwa hiyo tumekwenda vizuri kwenye Kiswahili tunaamini ni fursa nzuri ya kuanza kukuza lugha ya Kiswahili katika bara la Afrika
Wakati huo huo, Dkt. Ndumbaro aliongeza kuwa, katika mkutano huo nchi wanachama waliweza kuongelea agenda kuu za nchi wananchama wa ukanda wa maziwa makuu ambazo ni Amani, Utulivu na Usalama hususani katika eneo la mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Sanjari na hilo, nchi nyingi zimeusifu uongozi wa Rais wa DRC, Felix Tshisekedi kuwa tangu alipoingia madarakani amejitahidhi kuhakikisha kuwa kuna kuwa na amnai ndani ya DRC pamoja na majirani zake. Pia Uganda, Rwanda pamoja na Angola zimesifiwa kufanikisha kusaini makubalianao ya kuleta amanai kati ya Uganda na Rwanda.
Akiongea awali wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje Mgeni rasmi ambae alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kongo, Bwn. Clement Mouamba alisema kuwa mkutano wa leo, umelenga kuisaidia nchi ya DRC katika changamoto inazopitia hasa katika ukanda wa mashariki.
"Nawapongeza sana kwa kazi ambayo mmekuwa mkiifanya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa ugonjwa wa ebola unatokomezwa, kwani naamini kuwa umoja wetu tunaweza," alisema Mouamba.
Aliongeza kwa kuzitaka nchi wanachama wa ukanda wa maziwa makuu kuendelea kulinda amanai na umoja walionao ili kuweza kuendelea na shughuli mbalimbali za maendeleo kwani bila amani ni vigumu sana kwa umoja huo kuendelea.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikianao wa Jamhuri ya Kongo, ambae pia alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo Mhe. Jean Claude Gakosso aliwasisitiza mawaziri wa nchi wanachama kuwa amani na umoja katika ukanda huo ni nguzo muhimu sana na hivyo waendelee kuishika amani hiyo.
Pia aligusia ugonjwa wa ebola na kuwataka nchi wanachama kutokata tama ya kupambana na ugonjwa huo licha ya changamoto zinazojitokeza.
"Juhudi mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya DRC hadi sasa kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na wadau wengine katika kupambana na ugonjwa huo ni kutoa chanjo ya kinga ya ugonjwa huo na elimu kwa wananchi wa maeneo yaliyoathirika na ugionjwa huo" alisema Waziri Gakosso.
Mkutano wa leo ulitanguliwa na mikutano miwili ambayo ilianza tarehe 11 hadi 14 Oktoba 2019, jijini Brazzaville ambapo pamoja na mambo mengine ilijadiliwa suala la ugonjwa wa ebola na hali ya amani katika maeneo yenye mlipuko wa ugonjwa huo.
Nchi wanachama wa ukanda wa maziwa makuu ni pamoja na Angola, Burundi, Jamhuri ya Kati, Demokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Kongo, Kenya, Rwanda, Sudan, Sudani Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia.
Mwezi Augusti, 2019 Umoja wa Maendeleo ya Nchi za Ukanda wa Kusini mwa Africa (SADC) ulifanyika Tanzania Jijini Dar es Salaam nchi wananchama waliridhia na kuipitisha kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne ya Umoja huo baada ya Kiingereza, Kireno na Kifaransa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: