Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akitekeleza majukumu katika gari yake wakati wa ziara yake mkoani Tanga mwishoni mwa wiki. Wa pili kulia ni Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shighela, wa tatu kushoto ni Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daud Mayeji na wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Idara ya Mipago Miji Ofisi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini Nickson Mjema (Kulia).(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shighela (Kushoto) wakati akikagua moja ya itakayokuwa ofisi ya Ardhi mkoa wa Tanga wakati ziara yake katika mkoa huo mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daud Mayeji.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Mipago Miji Ofisi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini Nickson Mjema (Kulia) wakati akikagua moja ya sehemu ya kuhifadhia nyaraka za ardhi wakati akikagua inayotarajiwa kuwa ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga akiwa katika ziara yake mkoani humo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shighela.
Na Munir Shemweta, WANMM TANGA.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka Wakuu wa mikoa nchini kuhakikisha wanaharakisha uanzishwaji Ofisi za Ardhi za mikoa ili kusaidia upatikanaji huduma za ardhi katika mikoa hiyo.
Lukuvi alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki mkoani Tanga wakati alipokagua ofisi zinazotarajiwa kuwa za ardhi katika mkoa huo ikiwa ni utekelezaji wa agizo alilolitoa la kuanzisha ofisi za ardhi kila mkoa kwa ajili ya kusogeza huduma za ardhi kwa wananchi.
Katika Mkutano wa Wataalamu wa sekta ya ardhi uliofanyika hivi karibuni jijini Dodoma Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitangaza kuanzisha ofisi za ardhi katika kila mkoa ili kurahisisha huduma za sekta hiyo ambapo sasa zinapatikana katika Kanda tisa ikiwemo ile Maalum ya Morogoro.
Lukuvi alisema, uharakishwaji uanzishaji ofisi za ardhi katika mikoa utasaidia wananchi kupata huduma za ardhi katika mikoa yao tofauti za sasa ambapo hulazimu baadhi yao kutembea umbali mrefu kufuatilia nyaraka ofisi za kanda jambo aliloeleza linawakatisha tamaa.
Alimpongeza mkuu wa Tanga Martine Shighela kwa kuwa Mkuu wa mkoa wa kwanza kukubali na kupokea agizo la kuanzishwa ofisi hizo za ardhi mapema kwa lengo la kuhakikisha migogoro ya ardhi inaondolewa katika mkoa wake.
Alisema, pamoja na uwepo ofisi za Kanda ambazo baadhi yake zinahudumia zaidi ya mikoa miwili lakini kero kwa wananchi kuhusiana na masuala ya ardhi zinaendelea ndiyo maana Wizara yake imeona ianzishe ofisi za mikoa zitakazokuwa zikitoa huduma kama zile zinazotolewa katika kanda.
Alizitaja huduma hizo kuwa ni Upimaji, Uthamini, Mipango Miji, Usajili na Utoaji Hati za ardhi aliloueleza kuwa ulikuwa ukipatikana ofisi za kanda pekee jambo lililokuwa likiwalazimu wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo na kufafanua kuwa, uwepo ofisi za mikoa utaongeza ari ya wananchi kuchukua hati kutokana na ukaribu wa ofisi.
‘’Mtu atoke Korogwe afuate hati Moshi, trend ya kuchukua hati inapungua kutokana na umbali maana maeneo mengine mtu anavuka mikoa miwili kwenda kuifuata Hati na Kamishna aliyeko Moshi ni vigumu kusimamia mikoa iliyo mbali’’ alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, binafsi alitaka mikoa yote 26 kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa kufikia Oktoba mwaka huu na Hati zitolewe katika mikoa hiyo jambo alilolieleza kuwa litapunguza kero na kuongeza wigo mpana wa makusanyao ya kodi ya pango la ardhi.
Lukuvi alibainisha kuwa, baada ya kuanzishwa ofisi za mikoa sasa ramani zote na historia ya masuala ya ardhi katika mikoa husika zitarudi katika ofisi hizo na Wakuu wa Mikoa hawatakosa msaada katika masuala ya ardhi kwa kuwa watalaamu wa ardhi watakuwa wakifanya kazi chini yao.
Kabla ya kukagua ofisi hizo Waziri Lukuvi alielezwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shighela kuwa, mkoa wake ulipokea kwa shauku kubwa uamuzi wa Serikali kuanzisha ofisi za ardhi katika mikoa na tayari umeshatenga ofisi hizo kwa ajili ya kuanza kazi ili kupunguza migogoro ya ardhi pamoja na kusogeza huduma karibu kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daud Mayeji alisema, uanzishwaji ofisi ya ardhi katika mkoa wa Tanga utausaidia sana mkoa huo kwa kuwa wamekuwa wakitumia muda mwingi kushughulika na masuala ya ardhi na hufanya zaidi ya safari 50 katika kipindi cha miezi mitatu kufuata huduma ya ardhi katika ofisi za kanda zilizoko Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Jiji la Tanga, uwepo wa ofisi za Ardhi za Mikoa itakuwa rahisi kwa jiji lake kushughulika na masuala mengine badala ya kujikita katika ardhi pekee suala alilolieleza lilikuwa likichukua muda mwingi.
Toa Maoni Yako:
0 comments: