Ngariba mstaafu na mwezeshaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL),Hawa Njolo, akitoa elimu juu ya madhara ya ukeketaji kwa Wanawake waliohudhuria kliniki katika Kijiji cha Mughamo.Ngariba huyo alitoa ushuhuda kuwa ameachwa na mume kisa amekeketwa.
Mafunzo yakiendelea
Ngariba mstaafu na mwezeshaji kuhusu mila potofu ya ukeketaji na ukatili wa kijinsia, Hawa Njolo (wa pili kushoto mwenye kitambaa chekundu kichwani) akishiriki kutoa burudani muda mfupi baada ya kutoa elimu juu ya madhara ya ukeketaji na ukatili wa kinjisia kijiji cha Mughamo.
Kaimu Meneja Mtendaji wa Shirika la ESTL, Philbert Swai,akitoa elimu juu ya madhara ya ukeketaji na ukatili wa kijinsia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Msikii Wilaya ya Singida.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MADHARA yatokanayo na mila potofu ya ukeketaji yameanza kuchukua sura mpya kufuatia wanawake walio keketwa walio katika ndoa kuanza kupewa talaka na waume zao Mkoani Singida kwa madai kuwa hawana radha wakati wa kufanya tendo la ndoa.
Hayo yamebainika mkoani hapa juzi wakati Ngariba mstaafu Hawa Njolo mkazi wa Kijiji cha Sagara wilaya ya Singida akitoa ushuhuda katika mkutano wa hadhara kuhusu kupewa talaka na mume wake Sababu ikiwa ni kukeketwa.
Alitoa ushuhuda wake huo mbele ya wanawake wenzake waliohudhuria kliniki katika Kijiji cha Mughamo iliyoandaliwa na Shirika la Empower Society Transform Lives (ESTL).
Akifafanua alisema wakati akiishi na mume wake Babati mjini Mkoa wa Manyara, mume wake alianza tabia ya kutembea nje ya ndoa na mwanamke ambaye hakukeketwa.
“Habari hizo nilizipata kwa wasiri wangu na hakuchukua muda akawa ananifanyia vituko mara kwa mara lengo likiwa tutengane na alipoona hakuna dalili ya kuachana naye alinilima talaka”, alisema Njolo.
“Binafsi nilikuwa namheshimu sana mume wangu pamoja na ndugu zake kwani kwa usafi wa aina zote mapishi nilikuwa vizuri wala sikuwa mwanamke wa magenge”.
Akifafanua zaidi alisema kosa lililosababisha aachwe na mume wake ni kukeketatwa kwa madai kuwa alikuwa hasikii raha wakati wa kufanya tendo la ndoa.
Akiijengea nguvu hoja yake hiyo Njolo ambaye ni mwezeshaji wa shirika hilo alisema mbaya zaidi mwanamke aliyekeketwa na kisha kufanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua, sehemu yake ya siri (mbele) huondoka kwenye uhalisia wake na kubaki kama kopo ambapo husababisha wakati wa kufanya tendo la ndoa kukosa raha.
Ngariba huyo ambaye alirithi kazi hiyo kutoka kwa bibi yake alitoa ushuhuda huo ikiwa ni sehemu ya elimu juu ya madhara ya ukeketaji aliyokuwa akiitoa kwa baadhi ya wanawake waliohudhuria kliniki hiyo.
Mkazi mwingine wa Kijiji cha Mughamo Zanura Maulidi,alisema kuwa yeye pia ni mwaathirika wa kitendo cha kukeketwa.
‘Mwaka 2011 tulifunga ndoa na mume wangu (hakumtaja jina) na tukiwa katika ndoa kwa miaka nane mwenzangu kaoa mke wa pili ambaye hajakeketwa na mume wangu anadai anamvutia wakati wa tendo la ndoa” Zanura alisema kwa masikitiko.
Zanura ameomba mafunzo hayo au elimu hiyo itolewe pia kwa wanaume ili kupunguza kasi ya kuachwa wanawake waliokeketwa.
Kaimu Meneja wa ESTL, Philbert Swai, alisema mradi huo unafadhiliwa na The Foundation for civil society kwa shilingi milioni 60 kwa mwaka moja na malengo yake ni kushirikisha makundi mbalimbali ya kijamii kubuni njia za kudumu kutokomeza na kukomesha kabisa ukeketaji na kukatili wa kinjisia.
Toa Maoni Yako:
0 comments: