Ndugu zangu,

Nchi za Sadc ni marafiki zetu wa kweli. Nchi yetu itakuwa na ugeni mkubwa na wa kihistoria wakuu wa nchi 16 wanachama wa Sadc. Ni jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika. Tukio hili linetanguliwa na maonesho na mikutano midogo midogo. Wimbi kubwa lijalo hutanguliwa na mawimbi madogo madogo.

Ilivyo, jumuiya hii ya Sadc inakuw kwa kasi na kuwa nguzo muhimu ya kiuchumi. Tanzania chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Tano, Dr. John Pombe Magufuli, imepata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa mkutano huu wa 39 wa Sadc.

Naam, nchi za Sadc ni marafiki zetu wa kweli kwa vile tumekuwa pamoja tangu enzi za harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika. Tanzania chini ya Brigedia Hashim Mbita ilikuwa mwenyekiti wa nchi tano zilizokuwa mstari wa mbele kwenye mapambano hayo. Dar Es Salaam ikawa makao makuu ya kamati ya ukombozi wa Umoja wa Afrika wakati huo ukiitwa OAU.

Nchi za Sadc zimekuwa na uhusiano wa kirafiki wa miaka mingi. Zina historia ya kusimama upande mmoja wa mapambano.
Kwanini Mkapa Ataunguruma leo?

Historia ni Mwalimu Mzuri. Itakumbukwa, mwaka 1978, Julius Nyerere akiwa Mwenyekiti wa Nchi zilizo mstari wa mbele kwa ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika, alimwita Ben Mkapa kutoka kuwa Balozi Lagos na kurudi Dar Es Salaam kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje.

Zilikuwa ni zama za mapambano. Nyerere aliujua uwezo wa Ben Mkapa katika kujenga hoja, kwa kalamu na mdomo. Ben Mkapa alipata kuwa mwanafunzi wa Nyerere Pugu Sekondari na akawa mwandishi wake wa habari Ikulu.

Mwaka ule wa 1978 Julius Nyerere aliongozana na Mkapa kwenye msafara mmoja wa kwenda nchi za Magharibi kupambana kwa ajili ya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika. Ziara ile ilibatizwa jina’ Nyerere, Crusade For Liberation’( Kitabu chake ninacho kwenye maktaba yangu).

Hivyo basi, Ben Mkapa anaijua Sadc mwanzo- mwisho kama wanavyosema mitaani. Alikuwepo kwenye kujenga misingi ya uwepo wake. Ni kwa tafsiri hiyo, leo Mkapa ataunguruma na kulitumia jukwaa hilo kukemea sera za kibeberu katika kufanya biashara na Afrika. Atazitaka nchi za Sadc kuitumia Sadc kama muhimili muhimu wa ukombozi wa kiuchumi. Ni kwa nchi wanachama kuwa na sauti moja yenye nguvu.

Maggid Mjengwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: