Mkuu wa Kitengo cha Utafiti kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo akiwaeleza wafanyakazi wa Taasisi hiyo (hawapo pichani) kuhusu tafiti saba za magonjwa ya moyo zilizofanywa na Taasisi hiyo ambazo zitawasilishwa katika mkutano wa kimataifa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza utakaofanyika wiki ijayo nchini Zambia.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Happiness Swai akiwaeleza wafanyakazi wa Taasisi hiyo (hawapo pichani) kuhusu utafiti wa shinikizo la damu na tatizo la kisukari uliofanywa na Taasisi hiyo ambao ni moja ya tafiti saba za magonjwa ya moyo ambazo zitawasilishwa katika mkutano wa kimataifa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza utakaofanyika wiki ijayo nchini Zambia.
Wataalamu wa Afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambao walifanya tafiti saba za magonjwa ya moyo ambazo zitawasilishwa katika mkutano wa kimataifa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza utakaofanyika wiki ijayo nchini Zambia wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzielezea tafiti hizo kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam. Picha na JKCI.
Na Ales Mbilinyi – JKCI.
Tafiti saba za magonjwa ya moyo zilizofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) zinatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano wa wanasayansi, madaktari bingwa na wahudumu wa afya wanaotoka katika nchi za ukanda wa Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika utakaofanyika wiki ijayo nchini Zambia.
Tafiti hizo ambazo zimefanyika mwaka jana na mwaka huu ni kuhusu mwenendo wa mapigo ya moyo kwa mgonjwa, wagonjwa wenye moyo ambao uwezo wake wa kufanya kazi umepungua jinsi wanavyozingatia matibabu kama walivyoshauriwa na madaktari, shinikizo la damu na tatizo la kisukari.
Tafiti nyingine zitakazowasilishwa ni upungufu wa nguvu za kiume katika jamii, uelewa wa sababu hatarishi za magonjwa ya moyo katika jamii, magonjwa matatu kwa pamoja yaani moyo na figo kushindwa kufanya kazi na upungufu wa damu mwilini.
Akizungumza kuhusu tafiti hizo Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo alisema tafiti hizo zimefanyika katika mkoa wa Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka miwili na na kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
“Tumekuwa tukifanya tafiti mbalimbali kuhusu magonjwa ya moyo ambazo zinatusaidia kufahamu wagonjwa wetu pamoja na wananchi wanaotuzunguka wanakabiliwa na matatizo gani katika afya za moyo na hii inatusaidia kuweza kuboresha huduma zetu”,.
Akizungumza kuhusu mkutano huo wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza Dkt. Pedro alisema kwa upande wa magonjwa ya moyo utawasaidia kubadilishana matokeo ya huduma za matibabu wanazozitoa hasa tafiti zinazofanywa katika nchi mbalimbali ili kuboresha huduma zinazotolewa kwa wagonjwa. Kwa upande wake Afisa uuguzi wa JKCI Jalack Milinga ambaye alishiriki katika kufanya tafiti hizo alisema kwake ni mara ya kwanza kuhudhuria mkutano huo ambao utamsaidia kuongeza ujuzi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa moyo lakini pia kubadilishana uzoefu na wauguzi wenzake watakaoshiriki katika mkutano huo.
“Utafiti wangu uliangalia jinsi ya uzingatiaji wa unywaji wa dawa za moyo kwa wagonjwa ambao mioyo yao haifanyi kazi vizuri. Hivyo naamini ushiriki wangu katika mkutano huu utaniwezesha kupata mbinu mpya za kusimamia jukumu la kuwasaidia wagonjwa wetu kuzingatia matibabu ili kupata matokeo bora ya tiba”, alisema Jalack.
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Smita Bhalia alisema ushiriki wa wataalamu kutoka Tanzania umelenga kutoa matokeo ya utafiti uliofanywa hapa nchini na kuonesha baadhi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza jinsi yanavyoweza kusababisha magonjwa ya moyo ama magonjwa ya moyo yanavyoweza kupelekea mtu kupata magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza.
Malengo ya mkutano huo ni kwa nchi washiriki kutoka ukanda wa Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika kuona jinsi ya kushirikiana katika kufanya tafiti za ndani, kuwa na njia bora na za kisasa za matibabu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kuwa na mbinu mpya za kuweza kuzia magonjwa hayo.
Mkutano huo ambao hufanyika kila mwaka unatarajia kufayika mjini Living stone nchini Zambia kuanzia tarehe tano hadi saba mwezi ujao ambapo mwaka jana mkutano kama huo ulifanyika jijini Nairobi nchini Kenya.
Toa Maoni Yako:
0 comments: