Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio akikagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia viwandani kwa Mkoa wa Pwani, kulia ni Kaimu Meneja Mkuu wa GASCO, Mhandisi Baltazar Mrosso.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Meneja Mkuu wa GASCO, Mhandisi Baltazar Mrosso katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu Mkuranga.

Na Mwandishi Wetu.

Mkoa wa Pwani ni moja ya mikoa mitatu inayonufaika na matumizi ya gesi asilia viwandani, mikoa mingine ni pamoja na Mtwara na Dar es Salaam. Kwa mujibu wa taarifa kutoka TPDC, kuna viwanda vinne hadi sasa Mkoa wa Pwani ambavyo vimeshatiliana sahihi mkataba wa mauziano ya gesi asilia na TPDC.

Katika ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi zaidi kwa wateja wa viwandani mkoani Pwani, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio anasema “kuelekea Tanzania ya viwanda, TPDC inahakikisha upatikanaji wa nishati nafuu na rafiki kwa mazingira ili kuwezesha utekelezaji wa azma ya kuwa na Tanzania ya viwanda”.

Matumizi ya gesi asilia kwa viwanda vya Pwani ni takribani futi za ujazo milioni 4.7 kwa siku ambapo matumizi huongezeka kutokana na uzalishaji katika viwanda hivyo. “Mwanzo tulikuwa tukitumia mafuta mazito ambayo yalikuwa yakitugharimu milioni 200 kwa mwezi, matumizi ya gesi yanatugharimu milioni 80 kwa mwezi na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji kwa zaidi ya asilimia 50%” anaeleza Ndg. Raju Singh, Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Lodhia kinachozalisha bidhaa za chuma na plastiki.

Ndg. Raju alisisitiza pia kuwa matumizi ya gesi asilia yamepunguza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira ukilinganisha na mafuta mazito ambayo huzalisha kiwango kikubwa cha hewa ukaa.

Kwa mwaka huu wa fedha TPDC imejipanga kujenga miundombinu ya kuwezesha kuwaunganishia gesi asilia wateja wengi zaidi Wilaya ya Mkuranga na mpaka sasa viwanda vinne vimeshaonesha nia ya kutumia gesi hiyo, ilieleza taarifa kutoka kwa Dkt. Mataragio. Takwimu za TPDC zinaeleza kuna jumla ya viwanda 44 nchini vinavyotumia gesi asilia.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: