Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii

MAHAKAMA ya Rufaa, Tanzania imetupilia mbali maombi ya marejeo ya hukumu ya aliyekuwa Mkuu wa upelelezi Wilaya ya Kinondoni, Mrakibu wa polisi, Christopher Bageni aliyekuwa amehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua wafanyabiashara wanne wa madini kutoka wilaya ya Mahenge Mkoani Morogoro.

Kwa uamuzi huo ambao ndio wa mwisho, sasa Bageni hana namna nyingine ya kufanya kwani hakuna ngazi nyingine ya mahakama nchini wala hatua nyingine ambayo anaweza kuichukua kuupinga uamuzi huo, labda ikitokea neema ya Rais wa awamu ya sasa au awamu zijazo kumsamehe, kumwachia huru au kumbadilishia adhabu kama ataguswa au kuona kuna sababu ya kufanya hivyo.

Uamuzi huo umesomwa leo Agosti 14, 2019 na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufaa, Elizabeth Mkwizu baada ya mshtakiwa kushindwa kuishawishi mahakama kuwa ilikosea kumtia hatiani.

Mapema, mwaka 2016 Mrufani Bageni aliwasilisha maombi ya marejeo mahakamani hapo akiiomba mahakama hiyo ibadilishe uamuzi wake. Akiwasilisha hoja mbili kwamba, wakati mahakama inamtia hatiani ilizingatia ushahidi wa mshtakiwa mwenzie katika kesi ya mauaji ambae alikuwa ni mshtakiwa namba nne, ushahidi ambao hakuungwa mkono na shahidi yeyote mahakamani hapo ambapo kisheria mtu hawezi kutiwa hatiani kwa kutumia ushahidi wa mshtakiwa mwenzake isipokuwa kama utaungwa mkono na mtu mwingine.

Sababu ya pili alidai kuwa mahakama ilimnyima haki ya kusikilizwa na kuongeza kuwa wakati mahakama ya Rufaa inaamua rufani, kulijitokeza maelezo mapya ambayo hayakuwa kwenye ushahidi.

Akisoma uamuzi huo, Msajili Mkwizu amesema, mahakama imeangalia maombi ya mrufani na kwamba kuhusu hoja ya kuleta Maelezo mapya, Mahakama imeangalia ushahidi kwa makini na kugundua kuwa hakuna kitu kipya kwani mahakama inawajibu wa kuangalia kilichotokea ili kutenda haki na katika kuangalia ushahidi huo imeona hakuna mambo mapya.

Katika kufanya hivyo, mahakama haikufanya kosa lolote lililopelekea kuathiri haki ya mshtakiwa.

Akizungumzia juu ya hoja ya pili, Naibu Msajili Mkwizu amesema wakati Mahakama ya Rufaa inamtia hatiani mrufani Bageni, Ilizingatia ushahidi uliotolewa na Koplo Rajabu Bakari aliyeeleza kuwa Bageni ndiye aliyeamuru marehemu wale wapelekwe msituni na kwamba kule msituni yeye ndiye alikuwa afisa wa polisi mwenye cheo cha juu kuliko wote ingawa na ndiye alikuwa na uwezo wa kutoa amri.

Amesema, Koplo Bakari katika ushahidi wake alidai alimsikia Bageni akimuamuru mtu aliyetekeleza mauaji afanye hivyo. Shahidi huyo aliongeza kuwa hakuwepo eneo tukio lakini alisikia milio ya risasi ndipo akashuka kwenye gari na kwenda eneo la tukio ambapo alipofika alikuta marehemu wa NNE anauawa na mshtakiwa akiwa eneo la tukio.
Akichambua hilo naibu msajili amesena, kwa mujibu wa Sheria kuna namna nyingi za kuunga mkono ushahidi wa Koplo Bakari ikiwemo mienendo ya mshtakiwa alivyokuwa akionyesha baada ya tukio la mauaji.

Wameridhika kuwa ushahidi huo uliungwa mkono na namna Bageni alivyo "behave" baada ya tukio kwa namna mbili.

Kwanza alidanganya kwa wakubwa zake kwamba kulikuwaa na majibizano ya risasi kati ya polisi na majambazi kwenye ukuta wa posta sinza wakati mashahidi walioitwa kutoka sinza walisena hakukuwa na majibizano ya risasi.

Mbili. Bageni aliamuru askari wawili kwenda kufyatua risasi 9 baharini na akaja kuonyesha hayo maganda kuwa ndio yaliyopatikana posta sinza kwenye majibishano.

"Mtu yeyote anayedai Mahakama inakosea sehemu katika kufikia maamuzi yake, yeye ndie anayepaswa kuthibitisha madai yake lakini, mshtakiwa ameshindwa kuishawishi Mahakama kwamba ilikosea katika kufikia maamuzi iliyofikia ya kumtia hatiani, hivyo wao hawana namna nyingine zaidi ya kutupilia mbali maombi yake" amesema Mkwizu.

Uamuzi wa kutupilia mbali maombi hayo ya Bageni ulioandaliwa na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo waliosikiliza maombi hayo.

Jopo la majaji hao waliosikiliza na kutoa uamuzi wa maombi hayo namba 63 ya mwaka 2016 ni Stella Mugasha (kiongozi), Ferdinarnd Wambali na Rehema Kerefu.

Afisa huyo wa zamani wa Polisi alihukumiwa na mahakama hiyo adhabu hiyo Septemba 11, 2016, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam.

Alitiwa hatiani na mahakama hiyo kufuatia rufaa aliyoikata Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachia huru yeye na maafisa wenzake wengine wa polisi katika kesi ya msingi.

Lakini siku chache baadaye, alifungua maombi hayo akiiomba mahakama hiyo ifanye marejeo ya hukumu yake hiyo kisha imuondolee hatia na kumfutia adhabu hiyo na iamuru aachiwe huru, akidai kuwa hiyo iliyomtia hatiani ina kasoro za dhahiri.

Siku ya usikilizwaji wa maombi hayo, wakili wake Gaudiosus Ishengoma alidai kuwa mahakama hiyo ilimtia hatiani bila kumpa fursa ya kumsikiliza kwani ilimtia hatiani kwa ushahidi ambao haupo kwenye kumbukumbu za mahakama na wala haukujadiliwa kwenye rufaa ya DPP.
Hata hivyo mahakama hiyo katika uamuzi wake wa leo, imetupilia mbali sababu hizo ikisema kwamba hazina msingi kwa kuwa hoja zake hazina msingi kwa kuwa hakuna jambo jipya ambalo mahakama ililiibua na kwamba hakunyimwa haki ya kusikilizwa kwa kuwa alikuwa na wakili wakati wa rufaa hiyo.

Mkwizu alisema kuwa mahakama hiyo ilitekeleza majukumu yake na kwamba katika kumtia hatiani ilifanya tu uchambuzi wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani ukiwemo wa aliyekuwa mshtakiwa mwenza, aliyeeleza ukweli wa tukio na Bageni hakuupinga.
“Mwombaji ameshindwa kuonesha makosa kwenye hukumu hii (iliyomtia hatiani, kama alivyodai kwenye sababu zake za maombi.Kwa hiyo hatuna namna nyingine zaidi ya kuyatupilia mbali maombi haya, kwani.”, alisema Mkwizu. 

Katika kesi ya msingi, Bageni na wenzake 13, walikuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara hao Sabinus Chigumbi ( Jongo) na ndugu yake Ephrahim Chigumbi na mwenzao Mathias Lunkombe pamoja na Juma Ndugu, dereva teksi aliyekuwa akiwaendesha, Walikuwa wakidaiwa kuwaua kwa kupigwa risasi katika mstu wa Pande wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Januari 14, 2008.

Kabla ya kuuawa, walitiwa mbaroni na askari hao eneo la Sinza Palestina nyumbani kwa mchimbaji mwenzao, ambao waliwafunga pingu wakiwatuhumu kuhusika katika uporaji wa pesa za kampuni ya Bidco na baadaye polisi walidai kuwa walifariki wakati wakirushiana nao risasi.

Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa Agosti 17, 209 na aliyekuwa Jaji Kiongozi Salum Massati, aliyeisikiliza, ingawa alikiri kuwa kwa mujibu ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Bageni alikuwepo ndiye aliyeongoza msafara wa washtakiwa kwenda eneo la mauaji, lakini iliwaachia huru wote.

Jaji Massati alisema kuwa kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, mauaji hayo yalitekelezwa na Koplo Saad Alawi, ambaye hakuwa miongoni mwa washtakiwa (hadi sasa hajulikani aliko) na kwamba hakuna ushahidi kwamba Bageni aliamuru au alisaidia au aliwezesha mauaji hayo.

Lakini baada ya DPP kukata rufaa, Mahakama ya Rufani katika hukumu iliyotolewa na jopo la majaji watatu Bernard Luanda (kiongozi wa jopo), Sauda Mjasiri na Semistocles Kaijage ilimtia hatiani Bageni, na kumhukumu adhabu hiyo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: