Sehemu ya huduma mbalimbali kwa Wasafiri iliyopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataiafa Julius Nyerere Terminal 3, Jijini Dar es Salaam ambao ujenzi wake umekamilika hivi karibuni.

Na Lilian Shirima Maelezo.
 
Tanzania mpya imedhihirishwa na Ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria (Terminal 3) katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Akizungumza na Idara ya Habari Maelezo hivi karibuni Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa uwanja huo kutoka Wakala wa Taifa wa Barabara TANROADS, Mhandisi Barton Komba amesema:

“Jengo la tatu la Abiria limesanifiwa kwa viwango vya Kimataifa vya daraja C vya Usafiri wa Anga – IATA. Hivyo linatarajiwa kwa sasa kuwa kituo kikuu cha usafiri wa anga na kuleta tija kwa Tanzania”.

Mhandisi Komba ameongeza kwa kusema, asilimia 70 ya gharama ya mradi zimetumika kwenye usimikaji wa miundombinu ya mifumo maalum ndani ya jengo (airport special systems).

“Nasema ukizungumzia uwanja wa ndege, unazungumzia usalama wa abiria na mizigo, gharama iliyotumika katika usalama wa eneo la ndani ya jengo (Mechanical Eletrical Plumbing – MEP) pamoja na kufanyia kazi eneo la uhamiaji ambapo ni zaidi ya asilimia 70 ya mradi, mitambo ndio imechukua sehemu kubwa ya gharama.” 
Sehemu ya Ukaguzi mizigo kwa abiria yenye miundombinu ya kisasa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataiafa Julius Nyerere Terminal 3, Jijini Dar es Salaam ambao ujenzi wake umekamilika hivi karibuni.
Aidha, Mhandisi Komba amesema kuwa, katika eneo hilo sehemu ya uhamiaji kumefungwa madawati 10 yenye sehemu za kufanyia kazi 40 zenye uwezo wa kuhudumia abiria arobaini wanaowasili au kuondoka kwa wakati mmoja.

Mhandisi Komba amesisitiza kwa kusema kuwa kwa abiria ambao wanaotumia hati za kusafiria za kieletroniki (E Passport) hawatalazimika kupita kwenye huduma za uhamiaji bali kwenye lango la kieletroniki ( E-Gate) ambapo watahakiki hati zao za kusafiria na alama za vidole.

Pia, kwa upande wa ukaguzi wa mizigo (Baggage Handling System HBS) umesimikwa mfumo wa kisasa wenye uwezo wa kukagua mizigo katika madaraja matano tofauti pamoja na mashine za kukagua mizigo midogo ya mkononi . Ameainisha Mhandisi Komba

Komba amesema kuwa daraja la kwanza mzigo utaangaliwa kwa mashine (scanner) ili kubaini taswira ya kitu kilichomo ndani ambapo daraja la pili mzigo huo utachunguzwa tena kwa kutumia mashine (scanner) zenye nguvu zaidi ya kuona kwa kina.
Moja ya majengo yanayotumika kwa Abiria wanaondoka na wanaofika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere, Terminal 3, Jijini Dar es Salaam, ambao ujenzi wake umekamilika hivi karibuni.
Sehemu inayotumika kwa abiria kuingia na kutoka kwenye ndege yenye miundombinu ya kisasa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, kama inavyoonekana kwenye picha.

Daraja la tatu mzigo utachunguzwa kwa kutumia mashine zenye uwezo wa kuchanganua picha ya mzigo iliyoonekana kwenye daraja la pili kwa vipande mia moja tofauti (3 Dimention). Hatua itakayofuata ni mzigo utaingia daraja la nne sehemu ya wataalamu wenye uwezo wa kutasiri picha iliyoonekana katika madaraja yote yaliyotangulia.

Mhandisi Komba amesema, endapo mzigo hautakuwa na dosari ukifika daraja la nne utapata kibali na hivyo kuingizwa kwenye ndege. Aidha, mzigo wenye dosari utaingia daraja la tano ambapo hatua za kisheria zitachukuliwa na vyombo vya usalama.

Akifafanua Mhandisi Komba ameeleza kuwa eneo la kupokea mizigo lenyewe linayo mikanda minne yenye urefu wa mita 95, ukiwemo mmoja kwa ajili ya mizigo hatarishi inayotoka sehemu zisizokuwa na uhakika wa usalama kuingia kwenye nchi yetu. 

Akielezea miundombinu mingine Mhandisi Komba amesema “Miundombinu iliyosimikwa kwa viwango vya kimataifa ndani ya jengo hili ni mifumo ya tahadhari ya zima moto, utandazaji wa nyaya , ufungaji wa lifti na escalator pamoja na kazi nyingine za ndani ambazo kwa ujumla wake zimekamilika kwa asilimia 96.8”.

Kwa mujibu wa Mhandisi Komba, eneo la maegesho ya ndege na viungio vyake lenye ukubwa mita za mraba 227,000, limekamlika kwa asilimia 99.9 na kwamba ndege 19 za daraja C ambazo ni ndogo na ndege 11 za daraja E ambazo ni kubwa kama vile Boieng 787, Dreamliner zinaweza kuegeshwa kwenye eneo hilo. Tofauti ya ndege za daraja C na daraja E pia inatokana na urefu wa ndege, upana wa mabawa yake na vilevile ukubwa na idadi ya abiria. 

Amesema, Mhandisi Komba kuwa, kazi nyingine iliyokamilika na kuupa uwanja huu muonekano wa kimataifa ni usimikaji wa vivuko vya abiria 12 (Passanger Boarding Bridges) pamoja na ujenzi wa barabara za viungio kuingia na kutoka kwenye maegesho ya ndege. Kukamilika kwa mradi huu kunatarajiwa kuwa chaguo la ndege nyingi zinazoruka kwenda nchi za Afrika na bara Asia na Ulaya.

Eneo la nje ya jengo ambalo ni maegesho ya magari ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98.6 na ipo nafasi ya kuegesha magari 2,000 kwa ajili ya abiria wanaokuja na kuondoka nchini. Katika eneo hili imesimikwa mifumo ya kupoozea hewa na mifumo ya maji ya mvua na maji taka. Aidha, taa nyingi zimefungwa kwenye maegesho ya magari, jenerata 7 kwa ajili ya dharura kila moja ikiwa na uwezo wa 2MVA ili kuhakikisha huduma zinapatikana wakati wote hata inapotokea hitilafu ya umeme.

Akielezea historia ya uwanja wa ndege wa Kimatafa wa Julius Nyerere Mhandisi Komba amesema kuwa, ujenzi wa jengo la tatu la abiria ni mwendelezo wa majengo mawili ya abiria ya zamani yaani Terminal 1 na Terminal 2. Kilianza kufanya kazi mwaka 1959 kikiwa na jengo moja la abiria lenyw uwezo wa kuhudumia abiria laki 5 kwa mwaka na barabara moja ya kuruka na kutua ndege.

Jengo la Pili la Abiria (Terminal 2) lilijengwa mwaka 1984, likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria Milioni 1.5 kwa mwaka, idadi iliyofikiwa katikati ya miaka ya 2000. Hadi hii leo idadi ya abiria wanaohudumiwa katika uwanja wa JNIA imeongezeka na kufikia abiria Milioni 2.5 kwa mwaka. Kutokana na kuzidiwa kwa uwezo wa Jengo la Pili la abiria na kuzorota kwa huduma za abiria na mizigo kwasababu ya uchakavu wa jengo, mwaka 2000 wakati serikali ikiwa katika zoezi la uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ya viwanja vya ndege ilionekana dhahiri hitaji la ujenzi wa jengo jipya la abiria.

Aidha, wastani wa ongezeko la ongezeko la abiria wanaotumia kiwanja hiki ni asilimia 12.5 kwa mwaka. Ongezeko hili ndilo chimbuko la mradi wa ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria Milioni 6 kwa mwaka. Kukamilika kwa mradi huu kutawezesha uwanja huu kuwa kitovu cha usafiri wa anga kutokana na ukweli kwamba majengo yote  mawili terminal one na two yalikuwa yamezidiwa na wingi wa abiria wanaofikia Milioni 2.5 kwa mwaka. Amefafanua Mhandisi Komba.

Amemalizia, kwa kusema kuwa ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria (Terminal 3) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) unajengwa na Kampuni ya BAM International ya Uholanzi kwa gharama ya Euro milioni 276.7, sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 560 za kitanzania.
Uwanja wa JNIA umefikia asilimia 97.6 ya ujenzi na unatarajiwa kukabidhiwa rasmi kwa serikali mwishoni mwa mwezi Mei, 2019 ambapo uwanja una uwezo wa kuhudumia abiria milioni 6 kwa mwaka.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: