Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika Mheshimiwa Stephen Masele akiwa ofisini kwake, zilizopo Makao Makuu ya Bunge la Afrika, Jijini Johannesburg, Afrika Kusini akitoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Dr. Reginald Mengi.
Na Kadama Malunde – Johannesburg,Afrika Kusini.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika Mheshimiwa Stephen Masele amesema Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP marehemu Dr. Reginald Mengi ni Shujaa na Mwanamapinduzi wa kiuchumi na anastahili kupewa heshima ya kuwa Nembo ya Uwekezaji na Sekta binafsi Tanzania.
Mhe. Masele ambaye ni mbunge wa Shinyanga Mjini na Naibu Waziri wa Nishati na Madini wa zamani nchini Tanzania amesema hayo leo Jumapili Mei 5, 2019 akiwa nchini Afrika Kusini, wakati akitoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Dr. Reginald Mengi, aliyefariki dunia Mei 2, 2019 huko Dubai.
“Mzee Mengi ninamtambua kama Mwanamapinduzi wa Kiuchumi kwa sababu ndiye Nembo ya Uwekezaji kwa Wazalendo na ndiyo Nembo ya Sekta Binafsi katika nchi yetu”,ameeleza Masele.
“Mzee Mengi atakumbukwa zaidi kuwa miongoni kwa Watanzania wa mwanzo kuwekeza nchini na nitafurahi zaidi akipewa heshima ya kwamba yeye ndiye Nembo ya Uwekezaji,Nembo ya Sekta binafsi katika taifa letu”,amesema Masele.
Masele amemwelezea Mzee Mengi, kuwa alikuwa mtu mnyenyekevu,asiye na majivuno, mwenye kuheshimu watu wote bila kujali nafasi yake katika jamii licha ya kuwa na uwezo wake kifedha aliojaliwa na Mwenyezi Mungu.
“Nadhani ni vizuri kwa sisi vijana hususani viongozi kujifunza kwamba pamoja na nafasi tulizonazo ni vyema kuwa wanyenyekevu kwa binadamu wenzetu,mbele ya Mungu lakini pia kuheshimiana bila kujali nafasi zetu katika jamii”,ameongeza Masele.
Masele amewapa pole familia ya Mzee Mengi, marafiki,wafanyakazi wote wa Makampuni aliyokuwa anayaongoza na Watanzania wote kwa ujumla ikiwemo sekta binafsi.
“Kwa kweli nimepokea taarifa za msiba huu kwa huzuni kubwa,nimehuzunika kuondokewa Mzee wetu nilifanya nae kazi wakati nikiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na yeye akiwa kiongozi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania,tulifanya kazi kwa ukaribu sana,tulikuwa na vikao mbalimbali kuhusu masuala ya Uwekezaji.. tumuombe Mwenyezi Mungu ampe pumziko la amani Mzee wetu ,Amin”,ameongeza Masele.
Mheshimiwa Masele yupo Nchini Afrika Kusini kuhudhuria Kikao cha Pili cha Kawaida cha Bunge la Tano la Afrika kitakachoanza siku ya Jumatatu Mei 6, 2019 Jijini Johannesburg Afrika Kusini.
Mgeni rasmi atakayefungua kikao hicho cha Bunge la Afrika ni Spika wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Dk. Amal Abdulla Al Qubaisi ambaye tayari ameshawasili nchini Afrika Kusini.
Toa Maoni Yako:
0 comments: