Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikagua kiwanda cha nyama cha Meatco kilichopo jijini katikati mwa mji wa Windhoek Namibia. PICHA NA IKULU
Mhe. Rais Magufuli ametembelea kiwanda cha nyama cha kampuni Meatco kilichopo Jijini Windhoek na kuelezwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho Bw. Jannie Breytenbach kuwa kiwanda kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 630 kwa siku, kimeajiri wafanyakazi 650 na kwamba kampuni hiyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania kuanzisha viwanda vya nyama.
Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania ni nchi ya pili kwa idadi kubwa ya mifugo Barani Afrika na ameikaribisha kampuni ya Meatco kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Katika ziara hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina, Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.
Kabla ya kuondoka nchini Namibia kwenda nchini Zimbabwe ambako anakwenda kufanya Ziara Rasmi ya Kitaifa kwa mwaliko wa Rais wa Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Pili wa Namibia Mhe. Hifikepunye Pohamba Jijini Windhoek.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Windhoek
28 Mei, 2019
Toa Maoni Yako:
0 comments: