Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju ( katikati) akitoa maagizo nje ya gereza la Wanawake la WIlaya ya Musoma baada ya kutembelea gereza hilo kwa ajili ya kufanya ukaguzi na kuzungumza na wafungwa na mahabusu
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju ( alieshika fimbo nyeupe) ikiwa katika picha ya pamoja na timu ya wataalamu nje ya gereza la Wilaya ya Musoma mkoani Mara baada ya kufanya ukaguzi ndani ya gereza hilo na kuzungumza na wafungwa na mahabusu walioko ndani ya gereza hilo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju ( alieshika fimbo nyeupe) ikiwa katika picha ya pamoja na timu ya wataalamu nje ya gereza la Wilaya ya Tarime mkoani Mara baada ya kufanya ukaguzi ndani ya gereza hilo na kuzungumza na wafungwa na mahabusu walioko ndani ya gereza hilo.
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Bw. Biswalo Mganga (katikati ya Maaskari Magereza) katika picha ya pamoja na timu ya wataalamu nje ya gereza la Wilaya ya Mugumu- Serengeti mkoani Mara baada ya kufanya ukaguzi ndani ya gereza hilo na kuzungumza na wafungwa na mahabusu walioko ndani ya gereza hilo na kuwaachia huru mahabusu 66.
---
Mahabusu 201 waliokuwa katika magereza ya Wilaya za Musoma, Tarime na Mugumu Serengeti wamefutiwa kesi zao mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili kufuatia ziara ya ukaguzi ndani ya magereza hayo ya mkoa wa Mara iliyofanywa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Bw. Biswalo Maganga mwishoni mwa wiki iliyopita.

Viongozi hao walioambatana na wataalamu wao walifanya ukaguzi ndani ya magereza na kuzungumza na wafungwa na mahabusu walioko ndani ya magereza hayo nao ili kujua changamoto za kisheria zinazowakabili na kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinatatuliwa.

Baada ya kuzungumza na mahabusu hao na kupitia majalada yao Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Biswalo Mganga aliwaagiza waendesha mashtaka mkoa wa Mara kwenda Mahakamani na kuzifuta kesi zilizokuwa zikiwabili mahabusu hao ambao wataachiwa huru baada ya Mahakama kupokea nia ya DPP ya kufuta kesi hizo kwa mujibu wa sheria.

Mahabusu hao 29 wanatoka katika Gereza la Wilaya ya Musoma, 106 wanatoka katika Gereza Tarime na wengine 66 wanatoka katika Gereza Mugumu-Serengeti.

Katika Mahabusu hao wanawake ni 11, Watoto 39, wazee 9 na wanaobakia ni vijana ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi mbalimbali ambazo zilionekana zinaweza kumalizwa nje ya Mahakama, zile ambazo ushahidi wake ulionekana kuwa hafifu, kesi ndogo ndogo kama kupigana, kutukanana, wizi wa simu na vitu vingine vidogo vidogo, kutishiana kwa maneno, waliokiri kunywa gongo na kuvuta bangi, wengine walionekana kuwa mashahidi wa mashtaka.

Akizungumza na wafungwa na mahabusu katika nyakati tofauti ndani ya magereza hayo Naibu Katibu Mkuu Bw. Mpanju aliwataka mahabusu watakaofutiwa Mashtaka yao kubadili mienendo yao na kuwa raia wema na kuacha kuishi kimazoea kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria na Serikali haitoacha kuwachukulia hatua za kisheria.

“Ndugu zangu mmeona kazi kubwa tulioifanya leo hii humu ndani, ni wajibu wenu kuwa raia wema na kubadili mienendo ya maisha yenu, muache kuishi kwa mazoea, muangalie mnavyoishi na mkiachiliwa mkaambie na wenzenu kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria na Serikali haitawaacha lazima hatua za kisheria zichukuliwe”, alisema Bw, Mpanju.

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ambaye ni mratibu wa upelelezi wa kesi za jinai nchini Bw. Biswalo Mganga aliwataka wote wanaohusika na kazi ya upelelezi wa kesi mbalimbali zinazowakabili mahabusu hao kuhakikisha wanakamilisha upepelezi wa kesi mbalimbali kwa wakati ili kuondoa hali ya upelelezi kuchelewa.

Amesema kitendo cha kuchelewesha upelelezi kinawafanya watuhumiwa wa makossa ya jinai nchini kukaa magerezani kwa muda mrefu bila ya kujua hatma zao na hivyo kufanya magereza kuwa na msongamano ambao unaweza kuzuiliwa.

“Wapelelezi mlioko hapa, nadhani mnaelewa ninacho kisema hapa, fanyieni kazi haraka kesi za watuhumiwa hawa ili ziweze kumalizwa na wajue moja kama wanafungwa au wanaachiwa huru maana kwa kuendelea kuwa mahabusu hakuna tija kwa taifa, hawa watu humu ndani wanatakiwa wafanye kazi za uzalishaji na hiyo inakuwa sehemu ya urekebishwaji na sio kukaa bure na kujazana”, alisema Bw. Mganga

Mahabusu hao walikabidhiwa kwa mkuu wa upelelezi mkoa wa Mara ili kuhakikisha wanarudisha vitu walivyoiba, wanaombana misamaha na kuwa raia wema ndani ya jamii zao na kuambiwa kuwa Serikali itawachukulia hatua za kisheria tena iwapo wataenda uraiani na kujihusisha na vitendo vya kihalifu.

Katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu Mpanju aliongozana na wataalamu wa Sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Taifa akiwemo Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Dkt. Edson Makallo na Mkoa wa Mara, Maafisa kutoka Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Waendesha Mashtaka kutoka TANAPA.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: