Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Afya, mazingira na usalama migodini wa shirikisho la wachimbaji madini nchini (Femata) Dkt Bernad Joseph akizungumza na wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Ofisa madini wa mkazi wa Simanjiro Daudi Ntalima akizungumza na wachimbaji wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani.
Mwenyekiti wa Chama cha wachimbaji madini mkoani Manyara (Marema), Justin Nyari akitangaza matokeo ya uchaguzi wa Marema Tawi la Manyara, ambapo Shwaibu Mushi alichaguliwa kushika nafasi hiyo.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara Marema Tawi la Mirreani Shwaibu Mushi akiwashukuru wapiga kura waliomchagua kuwa Mwenyekiti wa Tawi hilo kwenye uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa diwani mstaafu Lucas Zacharia wa Kazamoyo Inn.
WANACHAMA wa chama cha wachimbaji wa madini Mkoani Manyara Marema Tawi la Mirerani Wilayani Simanjiro, wamechagua Mwenyekiti wao mpya, baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wao Samuel Rugemalira kujiuzulu nafasi hiyo hivi karibuni.
Mwenyekiti wa Marema mkoa wa Manyara, Justin Nyari akizungumza jana kwenye uchaguzi huo uliofanyika mji mdogo wa Mirerani alisema Shwaibu Mushi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Marema Tawi la Mirerani baada ya kuwabwaga wagombea wenzake watatu.
Nyari alisema Mushi alipata kura 36 na kuwabwaga wapinzani wake watatu akiwemo Hossea Palangyo Shilingi aliyepata kura 15, Abubakari Madiwa aliyepata kura tisa na Ramadhan Msumba aliyepata kura tano.
Hata hivyo alisema mgombea Hossea Palangyo (Shilingi) alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Marema baada ya kushika nafasi ya pili ya uenyekiti kwa kura 15 hivyo atajaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti ambayo awali ilikuwa inashikiliwa na Mushi.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo, Mushi alisema ataendelea kuifanya Marema kuwa bora zaidi ya jana na juzi.
Mushi aliwashukuru wale wote waliomchagua na waliompa ushirikiano kwenye nafasi ya Kaimu Mwenyekiti wa Marema wakiwemo viongozi wenzake wa ngazi ya Tawi, Mkoa na wachimbaji kwa ujumla.
Alisema ataendelea kuwa kiungo bora kati ya wachimbaji madini na serikali ili kuhakikisha madini hayo yanawanufaisha watanzania.
Kwa upande wake, Palangyo akizungumza baada ya kutangazwa kushika nafasi hiyo alisema yeye huwa anawajibika kwa wachimbaji na ataendelea kufanya hivyo huku akiwa na msimamo bila kuyumbisha au kuwayumbisha wachimbaji.
Hata hivyo, Ofisa madini mkazi wa Simanjiro Daudi Ntalima aliwataka viongozi hao wa Marema kutojiingiza kwenye unaharakati hivyo kutenganisha na shughuli zao za madini na kufarakanisha wachimbaji na serikali.
“Mimi ni mlezi wenu sasa ntashangazwa kama kuna baadhi ya viongozi wa Marema mnakuwa wana harakati na kuacha kufanya shughuli za kuwaunganisha wachimbaji na serikali na kujiingiza kwenye uanaharakati ambao hauna maana yeyote ile,” alisema Ntalima.
Toa Maoni Yako:
0 comments: