Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.

Mkurugenzi wa zamani wa Mipango, Ufutuatiliaji na Tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU, Kulthumu Mansoor, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya uhujumu ambapo anadaiwa kujipatia zaidi ya sh. Bilioni 1.4 kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kujipatia pesa kutoka kwa wafanyakazi wenzake sita.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa serikali Wankyo Simon amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Kelvin Mhina, kuwa, katika tarehe tofauti za Januari 2013 na Mei 2018, mshtakiwa alighushi barua ya ofa ya tarehe 13 Agosti 2003 kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa, barua hiyo imetolewa na Halmashauri ya wilaya Bagamoyo huku akijua kuwa siyo kweli.

Katika shtaka la kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu imedaiwa, kati ya Januari 2012 na Mei 2017 huko Upanga ndani ya Wilaya ya Ilala mshtakiwa kwa kudanganya alijipatia jumla ya sh. Milioni 32.2 kutoka kwa watu sita tofauti tofauti kama malipo ya viwanja tofauti vilivyoko Wilaya ya Bagamoyo katika kijiji cha Ukuni kwa kujifanya kuwa yeye ni mmliki wa kiwanja viwanja hivyo huku akijua kuwa sio kweli.

Mshtakiwa anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka kwa Alex Mavika ( milioni 5.2), Wakati Katondo, (milioni 3), Gogo James, (milioni 5), Ekwabi Majungu, (milioni 7) John Amos (milioni 7) na Rose Anatory, (milioni 5), ambao wote ni wafanyakazi wa Taasisi hiyo.

Katika shtaka la mwisho Imedaiwa kati ya Januari 2013 na Mei 2018 huku Upanga, mshtakiwa Kulthumu alijipatia kiasi cha sh.1,477,243,000 wakati akijua kuwa fedha hizo ni haramu na ni zao la kosa Tangulizi la kughushi.

Hata hivyo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina Mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo itatajwa tena Aprili 12.2019.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: