Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akieleza jitihada za Serikali katika kupambana na utapiamlo ikiwa ni pamoja na kila mkoa kuandaa bajeti ya lishe wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Binti Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe duniani, Sarah Zeid (hayupo pichani), Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Khatibu Kazungu na kulia ni Kamishna Msaidizi wa Bajeti wa Wizara hiyo Dkt. Charles Mwamwaja.
Binti Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya lishe duniani, Sarah Zeid, akieleza anavyofurahishwa na Serikali ya Tanzania inavyosimamia suala la lishe, wakati wa mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), kushoto ni Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani- WFP nchini Tanzania, Bw. Michael Dunford.
Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) Bw. Michael Dunford, akieleza utayari wa Shirika hilo kuisaidia Tanzania katika masuala ya lishe, wakati wa Mkutano kati ya Binti Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid (kushoto) na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia), na Ujumbe wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), ukiongozwa na Binti Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya lishe duniani, Sarah Zeid (wa pili kulia) katika mkutano kuhusu lishe, uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akipeana mkono na Binti Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe Duniani, Sarah Zeid (kushoto), baada ya kumalizika mkutano kuhusu Lishe uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Binti Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya lishe Duniani, Sarah Zeid (kushoto), wakifurahia jambo katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Tanzania na Shirika la Chakula Duniani- WFP, baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma. (Picha na Peter Haule, Wizara ya Fedha na Mipango).

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Binti wa Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid, ambaye ni Mwanaharakati wa masuala ya lishe, wanawake na watoto Duniani, jijini Dodoma.

Katika mazungumzo yao, Dkt. Mpango, alimweleza Princess Sarah Zeid kwamba Tanzania bado inakabiliwa na changamoto ya masuala ya lishe, utapiamlo na udumavu wa watoto licha ya nchi kuwa na chakula cha kutosha.

Dkt. Mpango alisema kuwa iwapo eneo la lishe halitasimamiwa kikamilifu Taifa litazalisha watoto wenye udumavu wa ubongo na kusababisha kupungua kwa uwezo wa kufikiri na utendaji hafifu wakiwa katika shughuli mbalimbali.

Alisema ipo mikoa ambayo inazalisha mazao mengi kama Mbeya na Njombe lakini ina kiwango kikubwa cha watoto wenye utapiamlo, na kutoa wito kwa kila mtanzania kuhakikisha anaangalia ni chakula gani kinahitajika kwa ajili ya lishe ya watoto na wakinamama wajawazito ili kupunguza udumavu na vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.

Aidha amempongeza Mwana wa Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid, kwa kampeni yake anayoifanya duniani kote kupambana na vifo vya wakinamama wajawazito na watoto kwa kuwa mchango wa wanawake ni mkubwa katika jamii ikiwemo uzalishaji mali.

Alisema idadi ya wanawake nchini Tanzania ni asilimia 51 ya idadi ya watu wote wanaokadiriwa kufikia milioni 55 ambapo mchango wako katika sekta mbalimbali za uchumi umekuwa mkubwa hivyo jitihada za kuwalinda zinahitajika.

Alimweleza Binti Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid kwamba kwa kutambua umuhimu wa lishe serikali imelivalia njuga suala la lishe kwa kutenga bajeti kila mwaka katika kila wizara na kwamba fedha hizo zimewekewa wigo zisitumike kwa matumizi mengine.

"Nimeziagiza Wizara, Mikoa na Halmashauri zote nchini kutumia fungu lililotengwa kwa ajili ya lishe kwa matumizi yaliyopangwa ili kuhakikisha watanzania wanaimarika kiafya na kushiriki kikamilifu katika Shughuli za Maendeleo" Alisema Dkt. Mpango.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango wakati wa Mkutano kati yake na Mwana wa Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe Dunia, Sarah Zeid na

Kwa upande wake Mwana wa Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid, ambaye aliambatana na Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) nchini Tanzania, Bw. Michael Dunford, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake katika kupambana na utapiamlo unaosababishwa na ukosefu wa lishe.

Amewataka watanzania kuhakikisha suala la Lishe linapewa kipaumbele na kila mmoja kwa manufaa ya Taifa na Dunia kwa ujumla na kwamba atahamasisha jumuiya ya kimataifa kuchangia jitihada za Serikali za kupambana na tatizo la lishe, na vifo vya wanawake wajawazito na watoto.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa-WFP nchini Tanzania Bw. Michael Dunford, amesema kuwa shirika lake linatambua mchango mkubwa wa Serikali katika kupambana na masuala ya lishe duni na shirika lake litaendelea kushirikiana na nayo ili kufikia malengo yanayotarajiwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: