Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete (pili toka kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji, Mhandisi Aron Joseph (mwenye tai) juu ya Mradi wa MajiSafi na Salama Mlandizi - Chalinze - Mboga, Pwani. Wengine ni Msimamizi wa Mradi huo Mhandisi Ishmaeli Kakwezi (kwanza toka kulia), Kaimu Mkurugenzi wa miradi DAWASA Lydia Ndibalema, Meneja Uhusiano wa Jamii wa (DAWASA) Neli Msuya (kwanza toka kushoto). Picha na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete akisoma ramani.
Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete (wa pili toka kushoto) akipata maelezo ya mradi toka kwa Msimamizi wa Mradi huo Mhandisi Ishmaeli Kakwezi (kwanza kulia).
Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete akikagua kiwanda kinachotengeneza mabomba ya kusambazia maji yatakayotumika kwenye mradi wa maji Mlandizi- Chalinze- Mboga, Pwani kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete (pili toka kulia) akipata maelezo kutoka kwa Afisa Utawala wa Kiwanda cha Mabomba cha TSP, Elly Bohela (mwenye kofi ya bluu) juu ya ubora wa mambomba hayo yanayopelekwa kwenye mradi wa kupeleka maji eneo la Mlandizi - Chalinze - Mboga, Pwani.
Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete akizungumza na wanahabari kuelezea juu ya furaha yake ya kuwapelekea maji wakazi wa Chalinze na vitongoji vyake.
Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji DAWASA, Mhandisi Aron Joseph, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa ziara ya Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete (kushoto) kwenye kiwanda cha Mabomba cha Tanzania Steel Pipes (TSP) kilichopo Ubungo Jijini Dar es Salaam leo.
Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete akijaribu kuendesha Lori lililokuwa limebeba baadhi ya mabomba ikiwa ni ishara ya kuzindua usafirishaji wa mabomba yatakayopelekwa katika Mradi wa Maji safi na salama wa Mlandizi - Chalinze - Mboga, Pwani.
Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete amefurahishwa na kasi ya utengenezaji wa mabomba ya kusafirishia maji yatakayotumika katika mradi wa maji wa Mlandizi-Chalinze - Mboga, Pwani.
Mabomba hayo yanatengenezwa na kiwanda cha mabomba cha Tanzania Steel Pipes (TSP) ambachoo ni cha wazawa kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam mpaka sasa yameshakamilishwa 321.
Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua ili kujionea kasi ya utengenezaji huo, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema kuwa imechukua miaka 16 kwa wananchi wa Chalinze kupata majisafi na salama na imani yake kubwa ipo kwa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA wafanikishe mradi huo.
Amesema, kukamilika kwa mradi huo ambao utachukua kipindi cha miezi mitano hadi sita utaweza kulinda kiti chake cha Ubunge kwani wananchi wamekuwa wanamsumbua kwa kipindi kirefu.
“Katika kukua kwangu sikuwahi kuona namna wananchi wavyotumia maji pamoja na wanyama kama ng’ombe ila kukamilika kwa mradi huu kutawawezesha watu wangu kupata majisafi na salama ila na wao kwa upande wao nitawaomba walipie huduma ili kuweza kuendesha miradi hii maji yaweze kupatikana,” amesema Ridhiwani.
Nae Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji, Mhandisi Aron Joseph amesema mradi huo utawanufaisha wakazi wa maeneo hayo ikiwa pamoja na wananchi wanaoishi kwenye eneo la mradi.
Mhandisi Joseph amesema Mradi wa maji wa Mlandizi -Mboga unatarajiwa kusafirisha maji lita milioni 9.3 (mita za ujazo 9300) kwa siku kiasi kianchokisiwa kuweza kutosheleza mahitaji ya walengwa kwa sasa na ongezeko la matumizi kwa siku za usoni.
“Hadi sasa, kiasi cha mabomba ya umbali wa km 3.7 yameshazalishwa katika kiwanda cha TSP na yameanza kupelekwa kwenye maeneo ya mradi ambapo ujenzi unatarajiwa kuanza katika Vijiji vya Mboga na Msoga,” amesema Joseph.
“Katika usanifu wa mradi huo, umetilia maanani ongezeko la watu na mahitaji ya miaka 20 ijayo na kutosheleza idadi ya watu hadi kufikia 120,912 ndani ya eneo la mradi na utakuwa kwa umbali wa Kilomita 58 ujenzi wa vituo viwili vya kusukumia maji na utagharimu bilion 14 hadi kukamilika kwake,” amesema Joseph.
Afisa Utawala wa Kiwanda cha Mabomba cha TSP, Elly Bohela amesema ametoa shukrani kwa Mbunge Ridhiwani Kikwete kufika katika Kiwanda chao kuona namna wanavyotengeneza mabomba hayo ambayo yanaenda kuwekwa kwenye mradi uliopo katika jimbo lake.
Amesema, kiwanda cha TSP ni cha wazawa na wamejizatiti kwenye kutengeneza mabomba yenye ubora aidha ameishukuru DAWASA kwa kuweza kuwaamini na kuwapatia kazi hiyo mahususi.
"Kiwanda Chetu kimeanza kufanyakazi tokea mwaka 2005 na tumekuwa tukitoa kipaumbele kwa mamlaka na taasisi za ndani ili ziweze kukamilisha miradi yao kwa wakati, hivyo muungano wetu huu na DAWASA utazaa matunda makubwa na pia tunakalibisha wadau wengine waje tuwapatie huduma," amesema Bohela.
Maeneo yatakayohudumiwa na mradi huo ni pamoja na Ruvu darajani, Vigwaza,Ranchi ya Taifa Ruvu (NARCO), Chahua -Lukenge, Visenzi, Buyuni na Mdaula-Ubenazomozi.
Vile vile maeneo ya Chamakweza, Pingi, Pera, Chalinze, Chalinze Mzee, Msoga na Mboga aidha, viwanda vitakavyofaidika ni pamoja na Twyford, kiwanda cha ngozi, kiwanda cha Matunda cha Sayona pamoja na watumiaji wengine wakubwa ikiwemo kampuni Yapi Merkezi wajenzireli ya kisasa (SGR).
Toa Maoni Yako:
0 comments: