Ugeni kutoka Brazili, Afrika Kusini, Kenya na Uganda ukiwa katika moja ya eneo lenye mradi wa majitaka wa simplified sewerage Jijini Mwanza. Huu ni ugeni wa pili kutoka nje ya Tanzania uliyotembelea mradi huo kwa Mwaka huu 2019.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) imepokea ugeni kutoka Asasi zisizo za Kiserikali kutoka Brazil, Afrika Kusini, Kenya na Uganda ambao umevutiwa na ubunifu uliyotumika katika ujenzi wa mradi wa Mfumo rahisi wa uondoshaji majitaka kwenye maeneo ya milimani unaofahamika kitaalam kama 'Simplified Sewerage System'.

Hayo yamebainishwa Machi 22, 2019 na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na masuala ya Kijamii nchini (CCI) Dkt. Tim Ndezi ambaye alikuwa mwenyeji wa ugeni huo kwa hapa nchini.

Dkt. Ndezi alisema mradi wa majitaka wa simplified sewerage umeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa mataifa mbalimbali kote ulimwenguni.

Alisema taasisi zinazojishugulisha na masuala ya usafi wa mazingira kutoka nchi mbalimbali baada ya kupata sifa za mradi huo wa Mwanza zimevutika kujifunza zaidi ubunifu uliotumika katika utekelezaji wake ili pia kuutumia katika nchi wanazotoka. "Wageni hawa wamekuja kujifunza namna ambavyo mradi huu umejengwa ili nao wakaandae mradi wa namna hii kwenye nchi zao," alisema Dkt. Ndezi.

Mradi huo wa Simplified Sewerage umeendelea kutembelewa na wageni kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kujifunza namna ukivyotekelezwa na namna ambavyo unaendeshwa.Kwa mujibu wa Dkt. Ndezi ni kwamna ugeni huo vilevile ulilenga kuzungumza na wanufaika wa mradi huo ili kufahamu wajibu wao na namna ambavyo waliupokea na njia wanazotumia kuutunza. 

Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu 2019 mradi huo kutembelewa na ugeni kutoka nje ya nchi kwani hivi karibuni MWAUWASA ilipokea ugeni kutoka Kenya ambao ulifika kwa ajili ya kujifunza namna bora ya kutekeleza mradi wa majitaka hususan kwa maeneo yasiyo rasmi. 

Ugeni huo wa awali kutoka Nchini Kenya ulieleza namna ulivyovutiwa na ubunifu mkubwa uliyotumika katika ujenzi wa mradi wa majitaka kwenye maeneo ya milimani na kuahidi kurejea tena na wataalam wa mamlaka zinazohusika ili kujenga miradi ya namna hiyo nchini mwao. 

Akizungumza mmoja ya wageni hao kutoka Uganda, Mundamba Omar alisema nchini humo ipo changamoto ya wananchi hususan wa kipato duni kukosa mfumo bora na rasmi wa uondoaji wa majitaka na kwamba ziara hiyo waliyoifanya Jijini Mwanza imewapatia uzoefu na ujuzi wa namna ya kujenga na kusimamia mradi mzuri wa majitaka. 

"Tunaipongeza MWAUWASA, kazi iliyofanyika hapa ni ya kipekee hatuna budi nasi kuiga," alisema Omar. Itakumbukwa kuwa Mradi huo wa Simplified Sewerage ulikuwa miongoni mwa miradi miwili bora zaidi kuwahi kutekelezwa Barani Afrika chini ya ufadhili wa African Infrastructure Trust Fund (EU-AITF).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendeji wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga ujenzi wa mradi huo ulianza Mwaka 2016 na umenufaisha Kaya zipatazo 415.Mhandisi Sanga alisema mradi huo wa Simplified Sewerage ulijengwa kwa majaribio kwenye maeneo matatu ambayo ni Kilimahewa, Mabatini na Igogo. 

Katika maeneo hayo matatu, Mhandisi Sanga alisema mwitikio ulikua mzuri na alitolea mfano kwa Kilimahewa ambapo MWAUWASA ilipanga kuunganisha Kaya 68 lakini kutokana na mwitikio kuwa mkubwa Kaya 117 ziliunganishwa na kwa upande wa Mabatini mpango ulikua ni kuungnisha Kaya 88 hata hivyo zaidi ya Kaya 178 ziliunganishwa na kufikia jumla ya Kaya 415 kwenye maeneo yote matatu.

Hata hivyo Mhandisi Sanga anabainisha kwamba awamu ya pili ya ujenzi wa mradi huo itahusisha maeneo mengi zidi ambayo ni Kabuhoro, Ibungilo, Kawekamo na Isamilo. 

"Maeneo ambayo tulianza nayo kwenye awamu ya kwanza nayo hatujamaliza, kwahiyo haya ni maeneo mapya lakini pia tutarudi kwenye hayo maeneo ya awali tukaunganishe Kaya zilizosalia," alibainisha Mhandisi Sanga. Akielezea sababu za mradi huo kuitwa simplified, Mhandisi Sanga alisema kwamba mradi ulipunguza baadhi ya vigezo kwenye miongozo ya usanifu miradi kutoka Wizara ya Maji. 

"Ukivifuata vigezo vyote kama vilivyo kwenye miongozo inakua ngumu kutekeleza mradi kwenye maeneo ya namna hiyo," alisema Mhandisi Sanga. 

Aliongeza kwamba changamoto iliyopo kwenye Jiji la Mwanza ni kwamba zaidi ya asilimia 70 ya maeneo hususan ya milimani hayajapimwa na hivyo kusababisha ujenzi wa miradi kuwa mgumu. 

Alibainisha kwamba kwa Tanzania, Jiji la Mwanza ni la kwanza kutekeleza miradi ya namna hiyo na kwamba kwa duniani miradi ya namna hiyo inapatikana Nchini Brazili. Mhandisi Sanga alisema lengo mahsusi la mradi huo ni kuondosha majitaka kwa njia rahisi kutoka kwenye maeneo ya milimani ili kuwaepusha wakazi na maradhi yanayoweza kutokea kutokana na mfumo usio rasmi wa uondoshaji wake. 

"Lazima tuhakikishe majitaka yanatolewa na yanatibiwa kwakuwa haya yanaweza kuwa ni hatari kwani mara nyingine hua ni chanzo kikuu cha maradhi," alisema. Alimalizia kwamba hapo awali uondoshaji wa majitaka kwenye maeneo ya milimani Jijini Mwanza ulionekana kuwa mgumu na kutowezekana." Ni lazima tuwe na majawabu kwenye maeneo ambayo hapo zamani ilionekana hayawezekani kabisa," alisema Mhandisi Sanga.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mbugani, Athumani Jama alisema hapo zamani kabla ya mradi hali ilikuwa ni chafu hasa ikizingatiwa hali halisi ya kijiografia ya maeneo hayo ya milimani. “Walikuwa wakichimba vyoo vifupi na wakati wa mvua hali inakuwa tete sana, maji yalikuwa yanatiririka ovyo na magonjwa ya mlipuko yalikuwa ya kufikia tu,” alisema Jama. 

Wananchi waliozungumza wakati wa ziara ya ugeni huo waliiomba MWAUWASA kuharakisha ujenzi wa mradi mpya ili Kaya nyingi zaidi zinufaike.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: