Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) wakipokea taarifa za maendeleo ya miradi ya gesi asilia jijini Dar es Salaam wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Dkt. Raphael Chegeni.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba (mwenye overall ya bluu) akiwaonyesha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya PIC kazi ya kusambaza gesi asilia kwa wateja kwa matumizi ya majumbani. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Raphael Chegeni.
Mhandisi Dora Ernest (alieshika mic ya TBC) akitoa maelezo ya huduma ya kusambaza gesi asilia kwa matumizi ya nyumbani kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC).
---
Kamati ya Bunge inayosimamia uwekezaji wa mitaji ya umma (PIC) imefanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya miradi ya gesi asilia jijini Dar es Salaam.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mhe. Dkt. Raphael Chengeni ilitembelea kituo cha kupokea gesi asilia Kinyerezi na kujionea kazi za kitaalam zinazofanywa na wazawa katika kupokea gesi na kuisambaza kwa wateja mbalimbali wakiwemo wazalishaji umeme.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba akitoa wasilisho juu ya mikakati ya TPDC katika kujiendesha kibiashara alisema “katika mwaka huu wa fedha tunategemea kuanza kutoa gawio Serikalini”. Mhandisi Musomba aliieleza Kamati ya PIC kwamba kwa sasa Shirika liko katika mageuzi makubwa ya kiutendaji nia ikiwa ni kuongeza ufanisi na hatimaye kutengeneza faida itakayoruhusu kutoa gawio kubwa Serikalini.
Katika kipindi cha miaka mitatu TPDC imekuwa ikijeindesha kwa hasara kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, Mh. Dkt. Raphael Chengeni alisema “Sisi kama Kamati tumefurahishwa sana na mageuzi makubwa ambayo yanaendelea kufanyika TPDC kwani hili lilikuwa moja ya Shirika ambalo linaonekana kuwa mzigo kwa Serikali kwa kushindwa kutoa gawio kwa Serikali”.
Dk. Chengeni aliongeza kwamba kwa taarifa waliyopokea TPDC sasa wanaamini mambo yatakuwa mazuri katika Shirika hili ambalo linategemewa sana katika kufikia Tanzania ya viwanda kwa kuzingatia upekee wa bidhaa wanayozalisha, gesi asilia. Wajumbe wengine wa PIC pia walionekana kuridhishwa na utekelezaji wa miradi na mageuzi ambayo TPDC imeshaanza kuyafanya.
Katika ziara hiyo Wabunge walipata nafasi ya kutembelea eneo la Ubungo na kujionea wa mtambo wa kupunguza mgandamizo wa gesi kwa ajili ya kusambaza kwa wateja wa majumbani na viwandani. Pia walitembelea maeneo ya Mlimani City na kujionea zoezi la kuunganisha gesi kwa wateja wa majumbani na baadae kiwanda cha Coca-Cola maeneo ya Mikocheni ambao nao wanatarajiwa kuanza kutumia gesi baada ya kazi ya kuunganisha kukamilika.
Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma inaangalia mambo matatu makubwa, kwanza gawio linalokwenda Serikalini, kupokea mtaji unaozidi na suala la mapato ghafi ambayo ni 15%, alieleza Mwenyekiti wa Kamati, Dk. Raphael Chegeni.
Toa Maoni Yako:
0 comments: