Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Moshi Selemani Kakoso, akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Bw. Masanja Kadogosa, wakati kamati hiyo ilipokagua hatua za maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam - Morogoro yenye urefu wa KM 300, eneo la Soga mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano), Atashasta Nditiye, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, ilipotembelea mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam - Morogoro yenye urefu wa KM 300, eneo la Soga mkoani Pwani.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Bw. Masanja Kadogosa, akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, wakati walipokagua hatua za mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam - Morogoro yenye urefu wa KM 300, eneo la Soga mkoani Pwani.
Meneja Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Dar es Salaam-Morogoro, Mhandisi Machibya Masanja, akielezea namna ya utandikaji wa reli hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, wakati ilipokagua mradi wa ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa KM 300 mkoani Pwani.
Muonekano wa sehemu ya Reli ya Kisasa iliyojengwa eneo la Soga Kibaha mkoani Pwani ambapo ujenzi wa mradi huu umefikia asilimia 45.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), unaoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa KM 300 na kusisitiza kuwa Bunge litaendelea kupitisha fedha za mradi huo hadi utakapokamilika kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Moshi Sulemani Kakoso, ameyasema hayo eneo la Soga mkoani Pwani mara baada ya kamati hiyo kukagua na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa katika mradi huo na kusisitiza kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuusimamia kwa ukaribu zaidi ili mradi uweze kukamilika kwa wakati .
“Kamati imekagua mradi na imeridhika na hatua za ujenzi wa reli hii hivyo hakikisheni unakamilika kwa viwango vinavyokubalika na ukabidhiwe mwishoni mwa mwaka huu kama mkataba unavyoelekeza”, amesema Kakoso.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa jitihada zinazoendelea kufanyika, Kampuni ya kikandarasi na wataalamu wote wanaosimamia ujenzi wa reli hiyo kwani kazi nzuri ya usanifu imefanyika ambapo baadhi ya madaraja magari yatapita chini na reli itapita juu na mengine reli itapita chini na magari yatapita juu.
Naye, mjumbe wa kamati hiyo Jafari Michael ambaye ni Mbunge wa Moshi Mjini, ameishukuru Serikali kwa hatua kubwa za ujenzi wa miundombinu ya reli hiyo kwa kuwa inapita katika mikoa sita yenye uzalishaji mkubwa wa mazao na chakula na pia itakuza uchumi wa nchi kwa kupata mizigo kupitia nchi jirani za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Naibu Waziri anayeshughulikia Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye, amesema kazi ya ujenzi wa tuta la reli umefikia asilimia 64 na miundombinu ya reli hiyo ishalazwa kwa zaidi ya KM 40.
Mhandisi Nditiye ametoa wito kwa wananchi kuitunza miundombinu ya reli kwani inajengwa kwa kutumia fedha nyingi na ni urithi kwa vizazi vijavyo na faida kwa Taifa.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea na utekelezaji sera ya kuwawezesha wakandarasi wazalendo ili kuwajengea uwezo katika ujenzi wa miradi ya kati na mikubwa ili kukuza uchumi wa nchi.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iko katika ziara ya kutembelea na kukagua miundombinu inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments: