Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokea Maandamano ya Timu za Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania wakati wa ufunguzi wa Michezo ya Majeshi kwenye Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam.
Kanda ya Ngome iliyojumuisha wachezaji wa Timu za Jeshi la Wananchi wa Tanzania {JWTZ} wakipita mbele ya Mgeni rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa ufunguzi wa Michezo ya Majeshi kwenye Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam.
Kanda ya Uhamiaji wakipita mbele ya Mgeni rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa ufunguzi wa Michezo ya Majeshi kwenye Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Tanzania Dr. Hussein Mwinyi akitoa maelezo ya kumkaribisha Mgeni Rasmi Balozi Seif kuyafungua Mashindano ya Michezo ya Majeshi Tanzania kwenye Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akihutubia wakati akiyafungua Rasmi Mashindano ya Michezo ya Majeshi Tanzania kwenye Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam.
Balozi Seif akisalimiana na Waamuzi wa Pambano kati ya Timu za soka za Ngome ya JWTZ na Jeshi la Kujenga Tatifa JKT zilizopambana katika siku ya mwanzo ya uzinduzi wa Mashindano ya Michezo ya Majeshi Tanzania katika Uwanja wa Uhuru Dar es salaam.
Baadhi ya Mawaziri wa SMZ na SMT, Makamanda wa Vikonsi vya Ulinzi na Usalama Tanzania Bara na Zanzibar wakifuatilia harakati za ufunguzi wa Mashindano ya Michezo ya Majeshi Tanzania kwenye Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo wa pili kutoka Kulia akiwaongoza Makamanda wa Vikosi mbali mbali vya Ulinzi na Usalama kushuhudia uzinduzi wa Mashindano ya Michezo ya Majeshi Tanzania kwenye Uwanja wa Uhuru.(Picha na OMPR-Zanzibar)
Na Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ongezeko la Mashindano ya Michezo ya ndani hapa Nchini ndio njia sahihi inayoweza kusaidia kutoa fursa pana kwa Wachezaji kujinoa vyema na hatimae kuongeza idadi ya Wanamichezo watakaoweza kushiriki vyema kwenye Michezo ya Kimataifa.
Alisema Michezo hivi sasa imekuwa chachu ya mafanikio kwa Mtu Binafsi, Taasisi na hata Taifa kwa vile tayari imeshaonyesha muelekeo mzuri wa kutoa ajira , amani, upendo, furaha, mshikamno pamoja na ushirikiano.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati akifungua mashindano ya Michezo ya Majeshi Nchini Tanzania inayoratibiwa na Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania { BAMMATA } inayofanyika katika Uwanja wa Michezo wa Uhuru Jijini Dar es salaam.
Alisema kitendo cha Viongozi wa Baraza la Michezo ya Majeshi {BAMMATA} kujipanga vyema kuandaa Michezo hiyo kimeleta faraja kwa Serikali kwa vile inaaminika kwamba hakuna jambo linaloshughulikiwa na Majeshi na baadae likafeli.
Balozi Seif alieleza kwamba Jamii inaelewa kwamba Wanamichezo wazuri Kitaifa na Wawakilishi wa Kimataifa mara nyingi hutokea katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama viliovyojijengea sifa na uwezo mkubwa kwa miaka mingi sasa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wanajeshi kutoliangusha Taifa linalojenga matumaini makubwa kwa Kundi hilo mahiri lenye uwezo mzuri wa kuipeperusha Bendera ya Tanzania Kimichezo katika Majukwaa ya Kimataifa.
“ Ni matumaini yangu kwamba Mashindano yajayo kama vile yale ya Majeshi ya Afrika Mashariki tutafanya vizuri zaidi kuliko tulivyoshiriki mara ya mwisho kwa kuwa sasa tumejifunza vizuri”. Alisema Balozi Seif.
Alisisitiza kwamba kwa vile Michezo hujenga Afya, Akili na Nidhamu ni vyema fani hiyo pia ikatumiwa katika kupambana na uhalifu kama vile vita vya kupambana na matumizi ya Dawa za kulevya pamoja na Mikakati dhidi ya udhalilishaji wa Wanawake na Watoto.
Akizungumzia umuhimu wa mazoezi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiasa Jamii kupendelea kufanya mazoezi ya kutosha katika muda wao za ziara ili kumkinga shetani kumruhusu kuyachota mawazo yao na kuyapeleka katika kufanya matendo maovu.
Alisema shetani anapaswa kunyimwa nafasi ya kumshawishi Mwanaadamu hasa Kijana kumpeleka kwenye matumizi ya dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia, ujambazi na badala yake ashiriki kwenye Michezo kikamilifu kama Sera ya Taifa ilivyoweka mkazo katika suala zima la kuimarisha afya kupitia michezo.
Alisema Wataalamu wa Afya Nchini wamekuwa akielezea uwepo wa ongezeko kubwa la maradhi yasiyoambukiza Nchini kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea kinachotokana na mfumo wa maisha wa kutumia zaidi vyakula vya makopo visivyokwenda sambamba na mpango wa mazoezi ya mwili.
Balozi Seif alisema Serikali zote mbili Nchini Tanzania ile ya Jamuhuri na ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa zikihamasisha Wananchi wake kufanya mazoezi pamoja na kutumia vyakula vya asili lengo likiwa ni kupambana na maradhi hayo.
Alitoa wito kwa Jamii kuendelea kuwa na Utamaduni wa kufanya mazoezi kwa kujihusisha katika michezo mbali mbali kwa ajili ya kulinda Afya zao pamoja na Uchumi kwa vile upatikanaji wa maradhi hayo tiba yake inakuwa gharama kubwa zisizoweza kumudiwa hasa na watu wenye kipato cha chini.
Akitoa Taarifa ya mashindano hayo Mwenyekiti wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania Kamanda Suleiman Mzee Mungea alisema Michezo hiyo imeasisiwa kwa lengo la kuwaandaa wanamichezo kuwa tayari katika kukabiliana na changamoto zozote zinazojitokeza.
Kamanda Suleiman alisema yapo mafanikio na faida kubwa iliyopatikana tokea kuanza kwa Michezo hiyo iliyopata umaarufu sana Nchini Tanzania licha ya changamoto zilizojitokeza za ufinyu wa Bajeti ya kuandaa Mashindano ya Michezo hiyo.
Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Generali Venance Salvatory Mabeyo alisema Sera ya Maendeleo ya Taifa inatoa fursa kwa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Nchini kushiriki katika Michezo wakati wa Amani.
General Mabeyo alisema Uongozi wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania {BAMMATA} umeamua kurejesha vugu vugu la Mchezo ndani ya Majeshi ili kurejesha hadhi yao ya ushiriki wa Mashindano ya Kitaifa na Kimataifa.
Alifahamisha kwamba ushiriki wa Wanamichezo wa Vikosi vya Ulinzi naUsalama ulififia katika Miaka cha nyuma kutokana na kukumbwa kwa changamoto kubwa la uhaba wa Bajeti katika kuwaandaa Wanamichezo wa Vikosi hivyo.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kuyafungua mashindano hayo ya Michezo ya Majeshi Nchini Tanzania {BAMMATA{ Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dr. Hussein Ali Mwinyi alisema Michezo ni sehemu ya Maisha ya Majeshi inayopaswa kuendelezwa na kudumishwa muda waote.
Dr. Hussein alisema Uongozi wa Vikosi vya ulinzi umeweka msukumo katika kuimarisha Michezo iliyoonyesha muelekeo mkubwa kwa Taifa la Tanzania kutambulika Kimataifa.
Mashindano hayo ya Michezo ya Majeshi Tanzania yameshirikisha Kanda Saba ambazo ni kutoka Kanda ya Ngome {JWTZ}, Kanda ya JKT, Kanda ya Polisi, Kanda ya SMZ, Kanda ya Magereza, Kanda ya Uhamiaji pamoja na Kanda ya Zimamoto.
Ufunguzi wa Mashindano hayo ulijumuisha burdani mbali mbali zilizotolewa Vikundi vya Utamaduni vya Sanaa Jeshi la Wananchi wa Tanzania {JWTZ}, JKT Sanaa, Polisi Jazzy Band pamoja na Kikundi cha mazingaombwe cha Kikosi cha Ngome.
Tumu za Mchezo wa Soka za Ngome ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania {JWTZ} na ile ya Soka ya Jeshi la Kujenga Taifa {JKT} zilimenyana ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa Michezo hiyo.
Timu hizo pinzani zilikutana katika Mchezo wa Fainali wa Mashindano ya Majeshi ambapo wababe wa Jeshi la Kujenga Taifa {JKT} walifanikiwa kuibuka na Ushindi dhidi ya Ngome kwa kuwalaza Goli 2-1.
Mashindano hayo ya 23 ya Michezo ya Majeshi Nchini Tanzania itafikia kilele chake Mnamo Tarehe 8 Mwezi Machi Mwaka huu wa 2019.
Toa Maoni Yako:
0 comments: