Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mwitikio wa Kitaifa,Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Bi Audrey Njelekela akifungua Kambi ya Watoto na Vijana ya Ariel 2018 katika hoteli ya Serene iliyopo Dar es salaam.Watoto na vijana hao wanatoka katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara.
Bi Audrey Njelekela akifungua kambi ya Ariel. Kutoka kulia ni Afisa Habari NACOPHA, Bi. Mensia John na Meneja wa Huduma za mama na mtoto AGPAHI Dk. Akwila Temu. Kutoka kushoto ni Meneja wa Fedha wa AGPAHI, Bw. Gwamaka Nsekela na Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa.
Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa, akizungumza katika ufunguzi wa Ariel Camp 2018 katika hoteli ya Serene, Dar es salaam.AGPAHI inatoa huduma za kisaikolojia kwa watoto na vijana wa mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mara na Mwanza kwa kushirikiana na serikali kupitia halmashauri za wilaya.
Vijana wakimsikiliza Dk. Sekela Mwakyusa.
Afisa Mradi wa Huduma za Jamii na Huduma Unganishi AGPAHI mkoa wa Mara, Madina Maduhu, akitoa historia fupi ya Klabu na Kambi za Watoto na Vijana. Alisema Kambi zilianza mwaka 2011 ambapo kikundi cha watoto 60 katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga kilianzishwa. Hadi Septemba 2018 kambi hizo zilifika 105 zikiwa na wanachama 4,320 katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mwanza na Mara.
Vijana na watoto wakifuatilia kilichokuwa kikiendelea ukumbini.
Kijana Agnes William akielezea faida za klabu za watoto na vijana. "Klabu za Ariel vinasaidia kuwajengea vijana na watoto uwezo wa kujieleza, kujitambua na ujasiri wa kuendelea na malengo yao ya maisha na kutimiza ndoto zao za baadae.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Babawatoto Centre, Bw. Mgunga mwa Mnyenyelwa akicheza na vijana na watoto.
Kikundi cha Taasisi ya Babawatoto kikitoa burudani ya sarakasi wakati wa ufunguzi wa Ariel Camp 2018.
Vijana wakifuatilia burudani.
Picha ya pamoja mgeni rasmi na washiriki wa Ariel Camp 2018.
Picha ya pamoja. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Imeelezwa kuwa vijana na watoto wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI wanahitaji msaada maalumu wa kisaikolojia kwa ajili ya kukabiliana na athari za kimwili, kisaikolojia, kijamii na kiroho ili waweze kuishi maisha marefu, yenye furaha na matumaini hivyo kutimiza ndoto zao.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatatu Disemba 10,2018 na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mwitikio wa Kitaifa, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Bi Audrey Njelekela wakati akifungua Kambi ya Watoto na Vijana ya Ariel 2018 katika hoteli ya Serene, jijini Dar es Salaam.
Kambi hiyo ya wiki moja inayojumuisha watoto na vijana 50 kutoka mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mara na Mwanza ambao pia ni wanachama wa klabu za vijana na watoto zinasimamiwa na asasi isiyo ya kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) inayolenga kutokomeza VVU na UKIMWI kwa watoto na familia.
Bi Njelekela alisema kuwa kupata tiba za kupunguza makali ya VVU pekee hakutoshi. " Watoto na vijana wanahitaji msaada wa kisaikolojia utakaowaimarisha ili kupambana na changamoto wanazokabiliana nazo," alisema.
"Changamoto hizi ni pamoja na msongo wa mawazo, unyanyapaa, hofu ya kufa au kujulikana kuwa wanaishi na maambukizi ya VVU, magonjwa ya kila mara na mshtuko unaotokana na kutunza wagonjwa au kushuhudia vifo vya wazazi au ndugu wa karibu," alieleza.
"Mara nyingi vijana wanaoishi na maambukizi ya VVU huwa wamepoteza mzazi mmoja au wawili, hivyo kutokuwa na watu wa kuwasaidia changamoto hizo na nyingine nyingi kuathiri makuzi na afya zao", aliongeza.
Aidha Bi Njelekela alisema ufuasi wa dawa za ARV ni mdogo sana miongoni mwa watoto ikilinganishwa na ufuasi wa dawa hizo kwa watu wazima. Alisema kuwa ili kukabiliana na hali hiyo msaada maalumu wa kisaikolojia ili kuwasaidia watoto ni muhimu.
“Ufuasi huo mdogo unaelezwa kusababishwa na watoto na vijana kutojua kwanini wanakunywa dawa na umuhimu wa dawa hizo kwa afya zao, shinikizo rika na kutokuwa na usimamizi wa kutosha,” alisema Bi Njelekela.
Bi Njelekela alitumia fursa hiyo kuipongeza na kuishukuru AGPAHI kwa kutoa elimu ya kisaikolojia kwa vijana na watoto na kuiomba pia itoe elimu hiyo kwa wazazi na walezi hasa ikizingatiwa kuwa wengi wao hawana elimu ya kutosha kuhusu VVU na UKIMWI.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa alisema wanaendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha maambukizi ya VVU yanatokomezwa.
“Tumeanzisha vikundi vya vijana wa umri balehe kwani tunatambua kuwa vijana wana mahitaji maalumu yanayoendana na ujana. Tumekuwa tukiwafundisha kuhusu masuala ya shinikizo rika, kujikinga na maambukizi mapya ya VVU, mabadiliko ya mwili, afya ya uzazi na stadi za maisha ili kuwajenga waweze kutimiza ndoto zao na kuwa wanachotaka,” aliongeza Dk. Sekela.
"Tanzania bila UKIMWI inawezekana hivyo tunaendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha tunawafikia watoto wengi waliozaliwa na maambukizi ya VVU tunawaanzishia huduma za tiba na matunzo," aliongeza Dk. Sekela.
Toa Maoni Yako:
0 comments: