Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Kampeni ya Siku 16 ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Baadhi ya Wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozindua kampeni ya Siku 16 ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Novemba 25, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (wapili kulia), Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa Nchini, Alvaro Rodriguez (kushoto) na Mratibu wa Kitaifa wa Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika ( WILDAF), Anna Kulaya wakati alipowasili kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kuzindua Kampeni ya Siku 16 ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia.
---
Serikali imesema imebadili utaratibu gerezani kwa watu watakaotumikia kifungo cha miaka 30 jela kutokana na kuwapa mimba au kuoa mwanafunzi.
Utaratibu huo uliobadilishwa ni wa kuhesabu siku, ambapo sasa mfungwa wa makosa hayo atahesabiwa usiku na mchana kuwa ni siku moja badala ya usiku na mchana kuwa siku mbili ilivyo kwa wafungwa wengine.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ndiye aliyefichua suala hilo jijini hapa jana, alipozindua Kampeni ya Siku 16 Kupinga Ukatili wa Kijinsia ambayo hufanyika kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10.
Kampeni hiyo imeratibiwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Akizungumza na wananchi katika uzinduzi huo, Majaliwa alisema serikali imewezesha marekebisho ya Sheria ya Elimu na kulifanya kosa la kumpa mimba kuoa au kuolewa mwanafunzi kuwa kosa la jinai na pale inapothibitika, adhabu yake ni kifungo cha miaka 30, hivyo watakaokutwa na mkono wa sheria "watakiona cha mtema kuni".
“Huwa nalizungumza hili, mtu yeyote atakayekutwa na tukamkamata amempa mimba, amemuoa, amemchumbia mwanafunzi, adhabu yake ni kubwa sana na kabla hujafanya tendo hilo jiulize una miaka mingapi ili ujue utakapoadhibiwa ukajumlisha na miaka yako tuone ukienda gerezani ujue unatoka na miaka mingapi," Majaliwa alisema na kuongeza:
"Kule gerezani tumesema utaratibu wa kuhesabu mchana na usiku kuwa ni siku mbili, kwenye adhabu hii ni siku moja tu, kama ni miaka 30 basi miaka 30 kweli, sasa je, miaka 30 utarudi ukiwa hai wewe?"
Waziri Mkuu aliwataka Watanzania kuwa macho na wale wote wasiowatakia mema wanafunzi, akiagiza kuwa "mtu akikutwa amesimama kwenye kona isiyoeleweka na mwanafunzi ashughulikiwe."
“Na wale wataalamu wa kuwasalimia wanafunzi mara nne nne kwa siku, ole wako tukikukamata utakiona cha mtema kuni, kwa hiyo eneo hili tumeimarisha kumlinda mtoto wa kike na serikali ya awamu ya tano imewekeza kwa mtoto wa kike," alisema.
Alisema mpango wa kufikia asilimia 50 kwa 50 utafikiwa kama ikiwekezwa kwa mtoto wa kike na serikali imedhamiria kufikia hatua hiyo.
Majaliwa alisema ukatili wa kijinsia hususan dhidi ya wanawake na watoto unarudisha nyuma juhudi za serikali za kuhakikisha kuwa mapinduzi ya viwanda na kilimo yanafikiwa.
“Hatuwezi kuwa na taifa linalozalisha na kufikia malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa kati iwapo muda mwingi unatumika kuamua migogoro na kuhudumia waathirika wa ukatili wa kijinsia badala ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji,” alisema.
Aliwaagiza wakuu wa mikoa kuhakikisha wanasimamia uanzishwaji wa kamati za ulinzi wa wanawake na watoto kwenye mikoa, halmashauri, kata na vijiji kama ilivyoelekezwa kwenye mwongozo wa uratibu wa mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
“Nawaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote kuanzisha programu za kijamii za kutokomeza ukatili wa kijinsia katika halmashuari husika zitakazozingatia hali halisi na kuzitengea bajeti programu hizo," alisema.
Majaliwa pia aliwataka wadau kutumia siku hizo kuwasilisha mapendekezo kama kuna upungufu unaohitaji sheria zitungwe kuwasilisha kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya kutunga sheria.
Waziri Mkuu pia alisema kumekuwa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayoleta madhara kwa jamii.
Aliagiza kila taasisi na kampuni ya simu kuhakikisha inawachukulia hatua kali dhidi ya watakaobainika wanatumia vibaya mitandao ambayo inarudisha nyuma jitihada za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“TCRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano) ambao ndiyo wanaofuatilia watumiaji wote wa mitandao, hakikisheni mnadhibiti na wale wote mnaojidanganya kuwa kuna mitandao haionyeshi, tukikukamata ndio utajua kuwa tunakuona," alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments: