Meli ya MV Mbeya II ikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi wake kwenye Bandari ya Kyela ambapo inatarajia kukamilika Mwezi Desemba Mwaka huu na itakuwa ikihudumia Abiria 200 na mizigo tani 200 kwenye Ziwa Nyasa.
Baadhi ya mafundi wa ujenzi wa Meli ya MV Mbeya II wakiendelea na kazi hiyo kwenye Bandari ya Kyela Mkoani Mbeya,kukamilika kwa ujenzi wa Meli hiyo kutasaidia usafirishaji wa Mizigo tani 200 na Abiria 200 kwenye Ziwa Nyasa.
Na Leonard Magomba
Kukamilika kwa ujenzi wa meli mpya ya abiria ya MV Mbeya II kunatarajiwa kutatua changamoto za usafiri wa abiria na mizigo katika mwambao wa Ziwa Nyasa.
Meli hiyo ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 80, itakuwa meli ya kwanza ya kisasa ya abiria ambayo itaunganisha mikoa mitatu ya Mbeya, Njombe na Ruvuma pamoja na nchi jirani za Malawi na Zambia.
Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa, Bw. Abed Gallus amesema kwamba ujenzi wa meli hizo ambao unafanywa na kampuni ya Kizalendo ya Songoro Marine, ni moja ya juhudi zinazofanywa na TPA kuboresha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo majini. “Ujenzi wa meli hii ya abiria, ni sehemu ya utekelezaji wa ujenzi wa meli tatu za TPA katika Ziwa Nyasa zilizolenga kutatua changamoto za usafiri wa abiria na mizigo majini,” amesema Gallus.
Bw. Gallus amesema kwamba TPA, ilianzisha mradi wa meli tatu zikiwemo mbili za mizigo zenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kila moja na moja ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200. Amesema kwamba miradi hiyo ilitekelezwa kwa awamu mbili tofauti ambapo awamu ya kwanza ilihusisha meli mbili za mizigo, MV Ruvuma na MV Njombe ambazo ujenzi wake ulikamilika mwezi Julai, 2017.
Ujenzi wa meli ya abiria ya MV Mbeya II ambao umefikia asilimia 80 unatarajiwa nkukamilika ifikapo mwezi Disemba, 2018 na umegharimu kiasi cha Tsh.9 bilioni za kitanzania. Asilimia 20 iliyobaki katika kukamilisha mradi huo wa meli inahusu ufungaji wa engine, generate, uwekaji wa vyumba na mambo mengine madogo madogo katika umaliziaji wa ndani na nje ya meli.
Meli hiyo ya abiria inatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa watumiaji wa usafiri wa majini kutokana na ukweli kwamba itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo na abiria kwa wakati mmoja. MV Mbeya II inatarajia kufanya safarinzake katika bandari mbalimbali kongwe na nyingine mpya zitakazoanzishwa na TPA katika mwambao wa Ziwa Nyasa ili kuleta ufanisi katika usafirishaji wa abiria na mizigo ziwani.
Toa Maoni Yako:
0 comments: