Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mtoto Sperius Eradius (13) aliyekuwa darasa la tano Shule ya Msingi Kibeta iliyopo Manispaa ya Bukoba, Kagera ambapo kimehusishwa na adhabu ya kupigwa na Walimu wake akiwa shuleni.

Kwanza, ninatoa pole kwa wazazi/walezi, ndugu na marafiki wa Mtoto Sperius Eradius. Poleni sana kwa msiba huu mzito, Mwenyezi Mungu awape moyo wa ustahimilivu. Apumzike kwa Amani mtoto Sperius.

Pili, Kufuatia wazazi wa marehemu kutokuwa na imani na uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera, Wizara yangu imetuma mtaalamu bingwa wa uchunguzi (Pathologist) toka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa ajili ya kwenda kufanya upya uchunguzi wa mwili wa marehemu na kubaini chanzo cha kifo hicho.

Tayari mtaalamu huyo ameshawasili Bukoba leo asubuhi kwa ajili ya kuanza uchunguzi. Ninatoa wito kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wananchi wote kwa ujumla kuwa watulivu kwenye kipindi hiki ambapo uchunguzi wa kibingwa unaendelea. Tutahakikisha kuwa uchunguzi unafanyika kwa ufanisi ili haki itendeke.

Tatu, nitumie fursa hii kuwakumbusha na kuwataka Wazazi, walezi na walimu kutambua kuwa tunaowajibu mkubwa wa kuwafundisha na kuwalea watoto wetu kwa kufuata sheria na taratibu tulizojiwekea katika jamii yetu. Ikumbukwe kuwa Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ikiwemo Vipigo havikubaliki katika jamii yetu na ni kinyume cha sheria za nchi. Kama jamii tunao wajibu wa kuhakikisha mtoto anaishi, kukua na kuendelezwa ktk mazingira salama na rafiki kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto No. 21 ya mwaka 2009. Nikiwa na dhamana ya kusimamia Sheria hii, NINALAANI VIKALI Vitendo vyote vya Ukatili vinavyofanywa dhidi ya watoto katika jamii. Hivyo tutaendelea kuwafuatilia na kuwachukulia hatua wale wote wanaoendeleza vitendo hivi.

Ummy Mwalimu, Mb.
WAMJW
Dodoma,
30 Agosti 2018
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: