Na Hussein Makame, NEC.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata 21 za mikoa 10 ya Tanzania Bara utakaofanyika tarehe 16 Septemba mwaka huu.
Akitoa taarifa ya uchaguzi huo jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Athumani Kihamia, alisema fomu za uteuzi wa wagombea wa uchaguzi huo zitatolewa kati ya tarehe 17 hadi 23 Agosti mwaka huu.
Aliongeza kuwa uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 23 Agosti wakati kampeni za Uchaguzi zitafanyika kati ya tarehe 24 Agosti hadi tarehe 15 Septemba mwaka huu.
Dkt. Kihamia alisema kuwa Tume imetangaza uchaguzi huo baada ya kupokea taarifa ya uwepo nafasi wazi za udiwani katika kata hizo 21 zilizopo katika Halmashauri 15 kutoka kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa.
“Nafasi wazi za udiwani katika Kata hizo zimetokana na sababu mbalimbali zikiwepo kifo, kujiuzulu, kutohudhuria vikao na kufutwa uanachama” alisema Dkt. Kihamia na kuongeza kuwa;
“Baada ya kupokea taarifa hiyo na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa; Tume ina utaarifu Umma kuhusu kuwepo kwa Uchaguzi mdogo katika Kata hizo 21.”
Kufuatia taarifa hiyo, Dkt. Kihamia alitoa mwaliko wa Tume kwa vyama vya siasa, wadau wote wa Uchaguzi na wananchi kwa ujumla kushiriki katika Uchaguzi huo.
“Tume inachukua fursa hii kuviasa vyama vya siasa na wadau wote wa Uchaguzi kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) za mwaka 2015” alisema Dkt. Kihamia.
Aidha alivitaka vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 pamoja na maelekezo yote yaliyotolewa au yatakayotolewa na Tume wakati wote wa Uchaguzi mdogo.
Uchaguzi huu mdogo wa udiwani katika kata 21 unatarajiwa kufanyika sanjari na uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Korogwe Vijijini, Ukonga na Monduli na kata za Tindabuligi na Kisesa katika Halmashauri ya Wilayani Meatu, uliotangazwa juzi ambao utakaofanyika siku ya Jumapili tarehe 16 Septemba mwaka huu.
Toa Maoni Yako:
0 comments: