Na Emmanuel J. Shilatu.
Watanzania tuna kila sababu ya kutembea kifua mbele kwani Mwenyezi Mungu ametupenda zaidi kwa kutupatia Rais John Magufuli ambaye ukitazama matendo, kauli na maisha yake yanaonyesha amejitoa kwa ajili ya Watanzania.
Dkt. Magufuli ni Rais wa kipekee ambaye amekataa kabisa kupanda ndege kwenda safari za kimataifa nje ya nchi na badala yake amewaachia wengine na yeye ameamua kujikita kutatua matatizo ya Wananchi. Katika hili Watanzania tumepata faida ya kupata Rais anayetumia vyema kodi zetu na si kuzifuja pia matatizo kumalizwa na maendeleo kupatikana kwa uharaka.
Ni Rais Magufuli huyu huyu ameamua kuthibiti rasilimali zetu ili ziwanufaishe Wananchi na si wajanja wachache. Rais Magufuli ameamua kuzuia usafirishwaji wa mchanga wa madini nje ya nchi, kujenga ukuta wa Mererani, kuzuia uchimbaji holela wa madini hali iliyozaa vita vya kiuchumi baina yetu na wale waliozoea kufaidi rasilimali za Taifa. Haya yote anafanya kwa niaba yetu Watanzania.
Bado wapo baadhi ya Watu wanamlaumu Rais Magufuli kuwa anapeleka pesa nyingi kwenye ujenzi wa miundombinu na kununua ndege! Tumeshajiuliza hiyo miundombinu inajengwa kwa faida ya Magufuli au ya Watanzania? Hizo ndege zinanunuliwa kwa faida ya Magufuli au ya Watanzania? Ndege zitapandwa na Watanzania wote, madaraja yatatumiwa na Watanzania wote, Reli ya umeme inapandwa na Watanzania wote na si kwa maslahi ya JPM. Tukishajua anafanya kwa maslahi ya Watanzania wala hatutaweza kulaumu chochote.
Wengine wanamlaumu Rais Magufuli kwa Serikali anayoiongoza kushupalia ukusanyaji wa kodi ambao wengine wanaona wanakamuliwa mno. Watu hao hao wanasahau ya kuwa anachokifanya Rais Magufuli ni kujenga uwezo wa ndani wa kifedha ili tuweze kujitegemea lakini kubwa tuweze kutekeleza vyema ilani ya uchaguzi ili Serikali iweze kujenga miundombinu, kupeleka huduma za kijamii kama umeme, maji na elimu bora na bure kila kona ya nchi. Rais Magufuli atawezaje kuendesha Serikali, kutoa elimu bure, kujenga miundombinu nk pasipo kukusanya kodi? Ni wajibu wetu kutambua kodi zinazokusanywa si kwa mkomoeni wala si kwa faida ya Rais Magufuli bali kwa faida ya Watanzania wote.
Rais Magufuli ameweka pembeni tabasamu kwenye mambo ya hovyo na badala yake amekuwa mkali pindi anapotaka kurekebisha masuala. Ameweka ukali kuwatimua wenye vyeti feki waliokuwa wanaziba ajira za Vijana wasomi; aliamua kufuta Watumishi hewa waliokuwa wanakula mishahara hewa na hivyo kufanikiwa kuokoa pesa walizokuwa wanalipwa; ameamua kuwatumbua watendaji wa hovyo na wabadhilifu wa mali za umma ili kujenga nidhamu ya uwajibikaji kazini.
Haya yote Rais Magufuli anayafanya si kwa maslahi yake bali kwa manufaa yetu Watanzania. Jambo tunalotakiwa kulifanya ni kumuunga mkono na kumuombea kwani ameonyesha nia, uwezo, dhamira safi na malengo chanya ya kiukombozi kwa Taifa letu kiuchumi.
Shilatu E.J
0767488622
Toa Maoni Yako:
0 comments: