Na Amini Mgheni.

Nimefuatilia kisa cha mwanafunzi huyu wa darasa la tano shule ya msingi Kibeta mkoani Kagera ambaye amefariki dunia baada ya kupigwa vibaya sana na mwalimu wa nidhamu shuleni hapo mwalimu Respicius Patrick (50) kisa na mkasa ni baada ya mwalimu Herieth Gerald kupoteza pochi yake na mwanafunzi huyo kutuhumiwa kuiba pochi.

Mwalimu huyu wa nidhamu alianza kumchapa mtoto Sperius Eradius (13) taarifa zinaeleza kuwa mwalimu alimpiga mwanafunzi huyu kila mahali kwenye mwili wake mpaka fimbo zikaisha akimshinikiza mtoto kusema pochi ameipeleka wapi.

Fimbo zilipoisha mwalimu alianza kuchukua kuni na kuanza kumpiga mwanafunzi huyo sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kichwani hali iliyomfanya mwanafunzi huyo kuishiwa nguvu na hapo baadaye kufariki dunia.

Mwalimu alimtesa mwanafunzi huyu mtoto mdogo kwa kila aina hadi mikono ya mwanafunzi huyu yote miwili ilivunjika mateso ambayo hakuna namna kuwa yalikuwa ya kiwalimu 

NAJIULIZA?

1. Baadhi ya walimu wetu tunaowakabidhi watoto wetu wamekuwa wanyama kiasi hiki? huyu mwalimu wala sio mwalimuwa kizazi hiki cha vijana wa siku hizi ana umri wa miaka 50 alisoma elimu ya mwalimu huyu.

2. Wakati Sperius Eradius (13) anapigwa kama mnyama kwa kiasi cha kifo walimu wengine walikuwa wapi shuleni hapo? walishindwa kumsaidia na kuona adhabu hii sasa ni ya kifo?

3. Jamii inayoishi jirani na shule hiyo ilikuwa wapi kusikia kilio kisicho cha kawaida hadi kuisha sauti cha Sperius Eradius (13) akiomba msaada wa kuokolewa mikononi mwa mwalimu aliyegeuka mnyama muuaji?

Baada ya kumpiga mwanafunzi na kumuua kwa kosa la kusingiziwa pochi ya mwalimu ililetwa shule na dereva wa bodaboda aliyetoa taarifa kuwa mwalimu aliisahau pochi hiyo ambayo Polisi wanasema ilikuwa na fedha taslimu elfu 75, simu ya mkononi kitambulisho cha mpiga kura na kitambulisho cha benki.

Nimewaza sana mpaka nimejikuta natoa machozi, uonevu mkubwa kabisa wa mtoto Sperius Eradius (13) aliyeuliwa kikatili na watu tuliowapa dhamana ya wakutunza watoto wetu, kinacho nisikitisha zaidi mtoto Sperius Eradius (13) ni yatima mama yake mzazi alifariki dunia baada ya kumzaa tu na alichukuliwa kwenye kituo cha watoto yatima na alikuwa akilelelewa na mchungaji.

Jibu rahisi tu tunamuhitaji Mungu kama jamii kuliko wakati mwingine wowote kwenye jamii yetu, jamii yetu imeonewa mno na shetani kiasi ambacho sasa unaweza kushuhudia kiwango chajuu kabisa cha unyama ambacho usingetegemea kufanyiwa na mtu,huku jamii ikiwa kimya kabisa na kutosaidia

Tuwakabidhi watoto wetu kwa Mungu wakati wote, tuombe kama taifa kukabidhi jamii yetu kwa Mungu muweza yote. Ili iwe salama na kurudishwa utu wa watu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: