NA RACHEL MKUNDAI, DAR ES SALAAM.

Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA imetangaza msamaha wa riba na adhabu za madeni ya nyuma ya Kodi hadi asilimia mia moja ili kutoa unafuu kwa walipakodi wenye malimbikizo kulipa kodi ya msingi tu yaani “Principal Tax”

Akitangaza msamaha huo, Kamishna Mkuu wa TRA Charles Kichere amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa msamaha huo ni matokea ya utekelezaji Maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika Mkutano wa Baraza la Wafanyabiashara (TNBC) uliofanyika Ikulu tarehe 20/03/2018 ambapo wafanyabiashara walilalamikia kuwepo kwa malimbikizo makubwa ya madeni ya kodi za nyuma yakijumuisha riba na adhabu,

Kichere amesema kuwa, ili kukamilisha hilo, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limefanya marekebisho kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2018 na sehemu ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015.

“Katika marekebisho hayo Waziri mwenye dhamana ya Fedha na Mipango amepewa mamlaka ya kutoa utaratibu maalum wa kuwezesha Kamishna Mkuu kutoa msamaha riba na adhabu wa hadi asmilia mia moja riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodikwa asilimia mia moja tofauti na asilimia 50 ya hapo awali”, amesema.

Aidha, amebainisha kuwa lengo kuu la msamaha huu ni kutoa unafuu kwa walipakodi wenye malimbikizo ya madeni ya riba na adhabu kwa kuwapa fursa ya kulipa malimbikizo ya madeni ya msingi ya kodi “Principal Tax” kwa awamu ndani ya mwaka wa fedha 2018/19 ili kuwapa motisha ya kulipa kodi kwa hiyari na kwa Wakati.

Amesema kuwa msamaha wa riba na adhabu utahusu kodi zotezinazotozwa kwa mujibu wa Sheria zinazosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, isipokuwa: Ushuru wa Forodha unaosimamiwa chini ya Sheria ya Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004; na malipo mengine yasiyo ya kodi ambayo TRA imepewa jukumu la kisheria la kuyakusanya. Mapato hayo ni kama vile: Kodi za Majengo na Ada za Matangazo.

Hata hivyo, Kamishna Mkuu wa TRA amesema kuwa watakaonufaika na utaratibu huu watatakiwa kuwa na sifa zifuatazo: Wawe wamewasilisha ritani za kodi lakini bado wanadaiwa kodi yote au sehemu ya kodi zitokanazo na ritani hizo; Hawajawasilisha ritani za kodi na wana madeni ya kodi; Ambao walikuwa wanafanyabiashara bila kusjiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), namba ya usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VRN) au usajili mwingine wa kodi kwa mujibu wa sheria zinazosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania;

Sifa nyingine ni wawe wamewasilisha pingamizi za kodi kwa Kamishna Mkuu na ambao pingamizi zao bado zinashughulikiwa katika ofisi za Mamlaka ya Mapato na sio kwenye mahakama za kikodi; Ambao wamewasilisha pingamizi katika mahakama za kikodi na mashauri yao bado hayajatolewa maamuzi na wale ambao wana madeni ya nyuma ya kodi ambayo hayatokani na kesi za jinai za kodi, utakatishaji Fedha, Usafirishaji wa binadamu au shughuli nyingine haramu.

Aidha, Mlipakodi atastahili kupata msamaha wa riba na adhabu endapo yeye binafsi au mwakilishi wake aliyeidhinishwa kisheria atawasilisha maombi ya msamaha kwa kujaza Fomu maalumu Na.ITX207.01.Einayopatikana katika tovuti ya TRA ikiambatana na; Maelezo ya kuonyesha kiasi anachodaiwa pamoja nakukubali kwa hiyari kulipa deni lake la msingi “Principal Tax” Kukubali kwa maandishi kulipa kiasi chote cha kodi bila riba na adhabu ndani ya mwaka wa fedha 2018/2019 ikiwa na maana kabla au ifikapo tarehe 30 Juni 2019; na Kwa madeni yaliyo katika pingamizi; kukubali deni la kodi alilokadiriwa na kuwa tayari kutoendelea na pingamizi au shauri husika la kodi lililowasilishwa kwa Kamishna Mkuu, Bodi ya Rufani za Kodi au Mahakama ya Rufaa.

Hata hivyo, msamaha utatolewa kwa maombi yatakayokidhi masharti na kukubaliwa na Mamlaka ya Mapato ambapo Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na Mlipakodi husika watasaini mkataba wa makubaliano utakaoanisha deni lote la kodi; riba na adhabu inayosamehewa, pamoja na kodi isiyo na riba wala adhabu itakayopaswa kulipwa kabla ya tarehe 30 Juni, 2019.

TRA inawahimiza walipakodi wote nchini kutumia fursa hii adhimu kwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hili maalum la utoaji wa msamaha wa riba na adhabu na kwamba utoaji wa taarifa sizizo sahihi ni kosa kisheria, endapo itabainika hivyo itapelekea muombajikupoteza sifa ya kufaidika na msamaha huu
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: