Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam.
Benki ya Credit Suisse ya nchini Uingereza imeonesha nia ya kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa zaidi ya Dola milioni 200 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo ikiwemo miradi mikubwa ya Nishati ya Umeme na miundombinu ya Reli.
Hayo yamebainishwa Jijini Dar es Salaam katika Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na Ujumbe wa Benki ya Credit Suisse ya Uingereza ulioongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Bw. Lawrence B. Fletcher, kuhusu ushirikiano katika miradi ya maendeleo.
Dkt. Mpango alisema kuwa tayari zipo hatua mbalimbalimbali zimefikiwa katika kufanikisha upatikanaji wa Mkopo kutoka Benki ya Suisse hivyo kuwa na tumaini la kupata kiasi cha Dola milioni 2000 katika mwaka wa fedha wa 2018/19 .
“Miradi ya Kipaumbele ambayo Serikali inaitekeleza ni pamoja na Ujenzi wa Reli kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), kufufua Shirika la Ndege Tanzania kwa kununua Ndege mpya na miradi ya umeme ambayo itachochea maendeleo ya watu na Taifa kwa ujumla”, alieleza Dkt. Mpango.
Aliitaja miradi mingine ambayo Serikali inampango wa kuitekeleza kuwa ni pamoja na Ujenzi wa Bwawa la Umeme la Rufiji (Rufiji Haydro Project) ambalo kukamilika kwake kutasaidia kuzalisha umeme wa Megawati 2100 ambao utatumika katika kuchochea uchumi wa viwanda unaohitaji umeme wakutosha.
Waziri Mpango amebainisha kuwa Serikali inatekeleza miradi ya kupanua Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Kigoma pamoja na ujenzi wa miradi mbalimbali ya barabara ambazo zitahudumia nchi ya Tanzania na nchi jirani ya Rwanda na Burundi hivyo kuchochea maendeleo.
Ameishukuru Benki ya Suisse, kwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya Maji, barabara na Umeme na kuahidi kuendelea kukuza ushirikiano na Benki hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Credit Suisse ya nchini Uingereza, Bw. Lawrence B. Fletcher, amesema kuwa Benki yake inaangalia uwezekano wa kufadhili miradi ya kipaumbele ya Serikali ili kuweza kufanikisha nia yake ya kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda.
Aidha amesema Benki yake itatoa mkopo wa Dola milioni 200 baada ya hatua za mkopo huo kukamilika katika mwaka huu wa fedha ili kuweza kufanikisha kutekeleza miradi mbalimbali lakini pia ikiwa ni sehemu ya kudumisha ushirikiano kati ya Benki yake na Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments: