Vodacom Tanzania Plc, kampuni pekee ya mawasiliano iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), imetambuliwa kama mmoja wa walipa kodi wakubwa nchini.
Utambuzi huu unaonyesha dhamira ya kampuni kuendesha biashara kwa uwazi, uwajibikaji na kwa kuzingatia sheria, huku ikichangia moja kwa moja katika maendeleo ya taifa kupitia ulipaji kodi na uwekezaji.
Akipokea tuzo ya mlipakodi mkubwa kutoka sekta ya Mawasiliano iliyotolewa na mamlaka ya mapato (TRA) jana jijini Dar es Salaam Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom alisisitiza kuwa mafanikio ya kampuni hayapo tu kwenye kutoa huduma za mawasiliano, bali pia katika kuchangia maendeleo ya taifa kupitia kodi, uwekezaji wa miundombinu ya kidijitali, ubunifu na kukuza rasilimali watu.

Kadri Tanzania inavyotekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Vodacom imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kuwekeza katika teknolojia za kidijitali, miundombinu ya mawasiliano na ujuzi, ili kuharakisha ujumuishi wa kidijitali na kukuza maendeleo jumuishi ya kiuchumi.
Kwa zaidi ya miaka 20, Vodacom imekuwa kichocheo cha mageuzi ya kidijitali nchini kwa kuunganisha watu, biashara na taasisi kupitia huduma za mawasiliano na suluhisho za kidijitali zinazoboresha maisha ya Watanzania na kuchangia ukuaji wa uchumi.




Toa Maoni Yako:
0 comments: