▪️ Waziri Mavunde akutana na mwekezaji wa kiwanda cha kuzalisha goroli za chuma
▪️ Kiwanda hicho kinatarajiwa kujengwa Buzwagi Special Economic Zone, Kahama
▪️ Oriental Casting and Forging Ltd ya China yajipanga kuwekeza nchini
▪️ Serikali yalenga kupunguza utegemezi wa bidhaa za migodini kutoka nje
▪️ Tanzania yajipanga kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za migodini Afrika
Dar es Salaam: Tanzania imeanza kujipanga kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za migodini barani Afrika, baada ya Serikali kuvutia uwekezaji wa viwanda vitakavyozalisha bidhaa muhimu zinazotumiwa na wachimbaji wakubwa na wadogo nchini.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, leo amekutana na Mkurugenzi Mkuu na mmiliki wa kampuni ya Oriental Casting and Forging Ltd ya China, Hou Songcun, kujadiliana kuhusu uwekezaji wa kiwanda cha kuzalisha goroli za chuma zinazotumika kusaga miamba ya madini katika shughuli za uchenjuaji.
Mavunde amewakaribisha wawekezaji hao kujenga kiwanda hicho katika eneo la Buzwagi Special Economic Zone lililopo Kahama, Shinyanga, ambalo Serikali imelitenga kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vinavyohudumia Sekta ya Madini.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji na sasa inalenga kuvutia viwanda vitakavyozalisha bidhaa za migodini ndani ya nchi, badala ya kuendelea kutegemea uagizaji kutoka nje.
“Lengo letu ni kuona wachimbaji wakubwa na wadogo hapa nchini wanapata bidhaa nyingi za kuzalisha madini bila kutegemea sana uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi,” amesema Mavunde.
Amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za migodini barani Afrika kutokana na ukuaji wa Sekta ya Madini, mahitaji makubwa ya bidhaa hizo na mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali.
Kwa mujibu wa Mavunde, uwekezaji wa viwanda vinavyohudumia Sekta ya Madini utaongeza ajira, kupunguza gharama za uzalishaji kwa wachimbaji, kuimarisha mnyororo wa thamani wa madini na kuongeza ushiriki wa viwanda vya ndani kwenye uchumi wa madini.
Amesema Serikali itaendelea kuvutia na kuunga mkono wawekezaji wanaolenga kujenga viwanda vinavyounganisha uchimbaji wa madini na uzalishaji wa bidhaa zinazotumika migodini, ili kuongeza manufaa ya sekta hiyo kwa uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Hou Songcun amesema kampuni yake iko tayari kufanya uwekezaji mkubwa nchini kwa kuwa Tanzania ina mazingira rafiki ya uwekezaji na Sekta ya Madini inaendelea kukua kwa kasi.
Amesema uzalishaji wa bidhaa za migodini ndani ya Tanzania utarahisisha upatikanaji wa vifaa hivyo kwa wachimbaji, kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa bidhaa muhimu katika shughuli za uchimbaji.
Kiwanda hicho kinatarajiwa kuongeza uwezo wa Tanzania kuzalisha bidhaa muhimu za migodini ndani ya nchi, kuimarisha viwanda vinavyohudumia Sekta ya Madini na kuiweka Kahama katika nafasi muhimu ya uzalishaji wa bidhaa za migodini kwa soko la ndani na la kikanda.






Toa Maoni Yako:
0 comments: