Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Tanzania Breweries PLC (TBL) imeendelea kuonyesha uimara wa biashara yake baada ya wanahisa kupitisha Ripoti ya Wakurugenzi, Ripoti ya Wakaguzi wa Hesabu na taarifa za fedha zilizokaguliwa za mwaka ulioishia Desemba 31, 2025, huku kampuni ikirekodi ongezeko la mapato na faida kutokana na ukuaji wa mauzo na uwekezaji wa kimkakati.

Maamuzi hayo yalifikiwa katika Mkutano Mkuu wa 53 wa Wanahisa uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, ambapo wanahisa walithibitisha pia mgao wa muda (interim dividend) uliolipwa kwa mwaka huo na kuidhinisha kampuni ya PricewaterhouseCoopers kuwa wakaguzi wa hesabu wa nje kwa mwaka wa fedha 2026.
Taarifa ya kampuni inaonyesha kuwa mwaka 2025 ulikuwa wa mafanikio makubwa, huku mapato yakiongezeka kwa asilimia 13 na faida ya uendeshaji kupanda kwa asilimia 35. Ukuaji huo umechangiwa na kuongezeka kwa mahitaji ya bia na vileo vikali, usimamizi madhubuti wa gharama, uwekezaji katika chapa mbalimbali pamoja na maboresho ya mfumo wa usambazaji wa bidhaa nchini.

Mwenyekiti wa Muda wa Bodi ya Wakurugenzi wa TBL, Balozi Ami R. Mpungwe, alisema Mkutano Mkuu wa Wanahisa umeendelea kuwa jukwaa muhimu la uwazi na uwajibikaji, huku ukitoa fursa kwa wanahisa kujadili utendaji wa kampuni na mwelekeo wake wa baadaye. Alisema Bodi itaendelea kusimamia kampuni kwa kuzingatia misingi ya utawala bora ili kulinda maslahi ya wanahisa na kuhakikisha ukuaji endelevu wa biashara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle N. Kilpin, alisema mafanikio ya mwaka 2025 yametokana na nguvu ya chapa za kampuni, imani ya wateja, ushirikiano wa wadau na utekelezaji makini wa mikakati ya biashara. Alibainisha kuwa kampuni itaendelea kuwekeza katika mifumo ya kidijitali, kuongeza matumizi ya malighafi zinazozalishwa nchini na kuboresha ufanisi wa shughuli zake ili kuimarisha ushindani sokoni na kuongeza thamani kwa wanahisa.

Mbali na matokeo ya kifedha, TBL iliendelea kuimarisha mchango wake katika uchumi wa ndani kupitia Kiwanda cha Kimea cha Kilimanjaro ambacho sasa kina uwezo wa kuzalisha tani 8,000 za kimea kwa mwaka, hatua inayoongeza matumizi ya shayiri inayolimwa na wakulima wa Tanzania. Kampuni pia imeendelea kupanua mfumo wa kidijitali wa kuagiza bidhaa, kuimarisha ushirikiano na wafanyabiashara wa rejareja na kuwawezesha wakulima wa shayiri na mtama kupitia mnyororo wa thamani.

Katika eneo la uendelevu, TBL ilieleza kuwa asilimia 92 ya vifungashio vyake sasa vinaweza kurejeshwa au kutengenezwa kwa malighafi zilizorejelewa, huku matumizi ya maji yakiendelea kuboreshwa katika shughuli za uzalishaji. Kampuni pia imeendelea kuhamasisha matumizi yenye uwajibikaji ya bidhaa zake na kutekeleza programu mbalimbali za maendeleo ya jamii na biashara, ikisisitiza dhamira yake ya kujenga thamani ya muda mrefu kwa wanahisa, wateja, wakulima na uchumi wa Tanzania kwa ujumla.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: