Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam. Kampuni ya Puma Energy Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake katika sekta ya nishati baada ya kutunukiwa Tuzo ya Rais ya Mlipa Kodi Bora katika kipengele cha Muagizaji Bora wa Mizigo ya Vimiminika (Best Wet Cargo Importer) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa hafla ya Tuzo za Rais kwa Walipa Kodi Bora iliyofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alimkabidhi tuzo hiyo mwakilishi wa kampuni kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hafla hiyo iliwakutanisha walipa kodi bora kutoka mikoa yote 35 ya Tanzania kwa lengo la kuhamasisha ulipaji wa kodi na kutambua mchango wao katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, alisema mafanikio hayo yanadhihirisha misingi imara ya uwajibikaji, uadilifu na uzingatiaji wa sheria ambayo imeendelea kuiongoza kampuni katika shughuli zake nchini. Alisema tuzo hiyo ni motisha wa kuendelea kuendesha biashara kwa uwazi, kulipa kodi kwa wakati na kushirikiana na Serikali katika kukuza uchumi wa taifa.
Fatma alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kampuni imechangia zaidi ya shilingi trilioni 1.4 kupitia kodi na tozo mbalimbali kwa Serikali, hatua iliyoifanya kutambuliwa mara kadhaa na TRA kwa utii wa sheria za kodi na mchango wake mkubwa katika kuongeza mapato ya ndani. Aliongeza kuwa kampuni itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya nishati na kupanua huduma zake ili kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali za uzalishaji.

Mbali na ulipaji wa kodi, Puma Energy Tanzania imeendelea kuimarisha uwekezaji wake kwa kuendesha zaidi ya vituo 100 vya huduma za mafuta, maghala ya kuhifadhi mafuta na usambazaji wa mafuta ya ndege katika viwanja vinane vya ndege, ikiwemo viwanja vyote vya kimataifa nchini. Kampuni pia inaongoza matumizi ya nishati safi kupitia Kituo Kikuu cha Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG Mother Station) pamoja na mtandao unaokua wa vituo vya CNG jijini Dar es Salaam na Morogoro.

Aidha, kampuni inaendelea kupanua huduma za gesi ya kupikia kupitia Puma Gas, biashara ya vilainishi na maduka ya Shop Express, huku ikiendelea kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji, ajira na huduma za nishati zenye ubora. Tuzo hiyo imeongeza hadhi ya Puma Energy Tanzania kama mmoja wa walipa kodi wakubwa na washirika muhimu wa Serikali katika kufanikisha ajenda ya maendeleo ya Taifa.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: