Na Jawadu kinyobwa - Dsm

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Wanafunzi wa sheria kujenga taaluma zao katika misingi ya nidhamu, ubunifu na uzalendo ili waweze kufanikiwa katika soko la ajira la kimataifa linalozidi kuwa na ushindani.

Akizungumza leo Juni 5, 2026 katika hafla ya Siku ya Kazi na Taaluma ya Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema mafanikio ya kitaaluma hayawezi kupatikana bila kuzingatia maadili hayo matatu muhimu.
Akifafanua kuhusu nidhamu, amesema ubora si jambo la muda mfupi bali ni tabia inayojengwa kwa kujifunza kwa bidii, kutunza muda, kuwa na hamu ya kujifunza mambo mapya na kuzingatia maadili ya taaluma. 

Amefafanua kuwa, nidhamu inayojengwa kupitia mahakama za mfano, kazi za kitaaluma na shughuli za msaada wa kisheria ndiyo msingi wa kukabiliana na changamoto za taaluma katika ngazi za kitaifa na kimataifa.
Aidha, kuhusu ubunifu, Waziri huyo amesema maendeleo ya teknolojia yamebadili kwa kiasi kikubwa namna taaluma ya sheria inavyotekelezwa duniani. Ametaja matumizi ya Akili Mnemba, mifumo ya kidijitali ya usajili na teknolojia za kisheria kuwa miongoni mwa mabadiliko yanayounda upya mazingira ya kazi za sheria. 

Katika hatua nyingine, amesisitiza umuhimu wa uzalendo, akieleza kuwa wao ni walinzi wa utawala wa sheria na utawala bora hivyo wanapopata fursa ya kufanya kazi katika taasisi za kimataifa au kampuni kubwa nje ya nchi, wanapaswa kutumia maarifa na uwezo wao kuisaidia Tanzania kutambulika vyema nje ya nchi.
Sambamba na hayo, Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha sekta ya sheria na haki kupitia mageuzi ya mfumo wa haki, matumizi ya teknolojia, uwekezaji katika miundombinu ya utoaji haki na kuhamasisha mifumo mbadala ya utatuzi wa migogoro.

Awali, akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mhe. Ridhiwani amesema sekta ya sheria ni nguzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia mchango wa wataalamu wa sheria katika kulinda maslahi ya taifa, kuimarisha utawala wa sheria na kusaidia mageuzi ya kidijitali.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: