Na Saidi Saidi, WMJJWM – Iringa

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Felister Mdemu, amewataka wanawake kushirikiana katika kujikwamua kiuchumi huku wakiendelea kuthamini familia, malezi bora, kuwaheshimu waume zao na kuhakikisha watoto wanapata malezi yenye maadili mema.

Mdemu amesema hayo mkoani Iringa, wakati wa mafunzo ya mwongozo wa uanzishwaji na uwezeshaji wa majukwaa ya wanawake kiuchumi yaliyofanyika katika Kijiji cha Kipaduka, Kata ya Uhambingeto, wilayani Kilolo. Mafunzo hayo yalihusisha madiwani pamoja na viongozi wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kutoka kata mbalimbali za mkoa huo.

Akizungumzia umuhimu wa majukwaa hayo, Mdemu amesema ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye lengo la kuwainua wanawake kiuchumi kupitia elimu ya fedha, ujasiriamali, matumizi ya teknolojia pamoja na upatikanaji wa mikopo na masoko.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wanawake kupata taarifa sahihi, kuunganishwa katika vikundi na kushiriki kikamilifu katika majukwaa hayo ili wasiachwe nyuma kutokana na ukosefu wa taarifa au usimamizi hafifu. Pia amewataka madiwani kushirikiana na taasisi za fedha, sekta binafsi pamoja na wataalam ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake katika maeneo yao.

Naye Diwani wa Viti Maalum kutoka Tarafa ya Kilolo, Mheshimiwa Julieth Mkolongo, akizungumza kwa niaba ya madiwani na viongozi wa majukwaa hayo, amesema wako tayari kutekeleza maelekezo yaliyotolewa ili kuhakikisha wanawake wanapata fursa za kiuchumi kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wao, baadhi ya wanawake walioshiriki mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata itawasaidia kuendesha vikundi vyao kwa ufanisi, kuongeza kipato pamoja na kuimarisha ustawi wa familia zao.



Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: