Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Waandaaji wa mbio za Run 4 Autism Tanzania Half Marathon 2026 wameweka wazi muongozo mpya wa ushiriki utakaozingatia makundi ya umri na viwango vya umbali, hatua inayolenga kulinda usalama wa washiriki na kuendana na kanuni mpya za riadha zilizoanza kutumika nchini kuanzia Januari 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Lukiza Autism Sports Foundation, mbio za watoto pamoja na watu wenye ulemavu hazitazidi kilomita mbili (km 2), kufuatia maelekezo ya kitaifa yanayokataza watoto kushiriki umbali mrefu zaidi ya huo. Kundi hilo linalenga zaidi watoto wenye umri chini ya miaka 12, huku watu wazima wanaoruhusiwa kushiriki katika mbio hizo wakiwa ni wale wanaoambatana na watoto wadogo.
Aidha, watoto wenye umri kati ya miaka 13 hadi 17 watashiriki mbio za kilomita tano (km 5), wakati washiriki wenye umri wa miaka 18 na kuendelea watakimbia mbio za kilomita 10 pamoja na nusu marathon ya kilomita 21.1.
Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Aprili 4, 2026 katika viwanja vya Shule ya Msingi Oysterbay jijini Dar es Salaam, zikiwa na lengo la kuhamasisha uelewa wa ugonjwa wa Usonji (Autism) pamoja na kuhimiza ushiriki wa jamii katika michezo kwa ajili ya afya na mshikamano.
Waandaaji wameeleza kuwa mabadiliko hayo si tu yanazingatia kanuni mpya, bali pia yanahakikisha kuwa kila mshiriki anapata uzoefu salama na unaofaa kulingana na umri na uwezo wake.
Sambamba na maandalizi hayo, washiriki wote wametakiwa kufika Mlimani City kwa ajili ya usajili na kuchukua vifaa vya kushiriki mbio hizo mapema kabla ya siku ya tukio.
Uongozi wa Lukiza Autism Sports Foundation umetoa shukrani kwa wadau na jamii kwa kuendelea kuunga mkono tukio hilo, huku ukitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo ambazo pia zinabeba ujumbe mpana wa kujali na kuunga mkono watoto wenye mahitaji maalum.
Mbio za Run 4 Autism zinatarajiwa kukutanisha wanamichezo, familia, wadau wa afya na wananchi kwa ujumla, katika jukwaa la kipekee linalochanganya michezo, elimu na mshikamano wa kijamii.



Toa Maoni Yako:
0 comments: