

Rais wa William Ruto wa Kenya amesaini rasmi sheria ya kuanzishwa kwa National Infrastructure Fund, hatua inayotajwa kuwa miongoni mwa mipango mikubwa zaidi katika historia ya maendeleo ya taifa hilo.
Hafla ya utiaji saini wa muswada huo imefanyika katika State House Nairobi mbele ya viongozi wa sekta ya biashara na uwekezaji kutoka Kenya, Afrika na sehemu nyingine za dunia.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Ruto alisema kuanzishwa kwa mfuko huo ni hatua muhimu katika safari ya kubadilisha uchumi wa Kenya kwa kuwezesha nchi kujitegemea katika kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo ya miundombinu.


Kwa mujibu wa Rais Ruto, fedha hizo zitawezesha utekelezaji wa miradi kadhaa ikiwemo uzalishaji wa megawati 10,000 za nishati safi, ujenzi wa mabwawa makubwa 50, mabwawa ya kati 200 pamoja na zaidi ya mabwawa madogo 1,000.
Aidha, alisema mfuko huo utasaidia kujenga kilomita 2,500 za barabara za njia mbili (dual carriageways) na zaidi ya kilomita 28,000 za barabara za kawaida ili kuboresha usafiri na uchumi wa nchi.


Pia serikali imepanga kutumia mfuko huo kugharamia upanuzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway kutoka Naivasha hadi Malaba na Kisumu, pamoja na kupanua uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta International Airport uliopo jijini Nairobi.
Rais Ruto alisema mfuko huo utaisaidia serikali kupanga vipaumbele vya maendeleo na kuvigeuza kuwa miradi inayoweza kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Aliongeza kuwa mfumo huo wa ufadhili si wa majaribio, bali umefanikiwa katika nchi nyingine duniani, na unaipa Kenya nafasi ya kusonga mbele kuelekea hadhi ya uchumi wa nchi zilizoendelea.
Rais huyo alisisitiza kuwa hatua hiyo pia ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na serikali yake kwa wananchi wa Kenya katika ilani ya uchaguzi.





Toa Maoni Yako:
0 comments: