Na Mwandishi Wetu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amekutana na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe.Ali Mwadini, kujadili mikakati ya kuvutia na kutafuta wawekezaji katika eneo la Bonde la Msimbazi lililopo jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamekubaliana kuwa na mpango madhubuti wa kutafuta wawekezaji wa kimataifa watakaoshiriki kuwekeza katika maendeleo ya bonde hilo, ambalo Serikali imeanza kulijenga ili kupunguza athari za mafuriko na wakati huo huo kufungua fursa mpya za uwekezaji na biashara.
Utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, kuboresha huduma za kijamii pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi wa jiji la Dar es Salaam na maeneo jirani, huku pia ukivutia wafanyabiashara na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Prof. Shemdoe amefanya ziara katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa jana Machi 13, 2026, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha uwekezaji unaofanyika katika Bonde la Msimbazi unaleta manufaa makubwa kwa uchumi wa taifa na kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara wa jijini Dar es Salaam.
Uwekezaji unaotarajiwa katika bonde hilo ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuendeleza miundombinu ya kisasa mijini, kudhibiti mafuriko na kuifanya Dar es Salaam kuwa kitovu muhimu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments: