
Wasanii kutoka Jamhuri ya Korea wakionesha moja ya ngoma za aslili za nchi hiyo wakati wa Tamasha la Ngoma za asili za Jamhuri ya Korea jana Jijini Dar es Salaam.
Na Dotto Mwaibale
Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa tukio kubwa la kimataifa la utamaduni litakalojulikana kama International Cultural Summit, litakalofanyika kwa siku sita kuanzia tarehe 16 hadi 21 Mei 2026. Tukio hilo litawaleta pamoja washiriki kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuonesha na kusherehekea utofauti wa tamaduni mbalimbali duniani pamoja na tamaduni za wenyeji.
Kongamano hili litaandaliwa na Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania (UNESCO National Commission of the United Republic of Tanzania) kwa kushirikiana na mwenyeji wake ambaye ni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya Zanzibar.
Lengo kuu ni kuimarisha uelewano wa kitamaduni, kukuza amani katika jamii zenye tamaduni tofauti na kutoa jukwaa la ubunifu kwa wasanii na wadau wa utamaduni.
Katika kipindi chote cha siku sita, washiriki kutoka Tanzania na wageni watapata fursa ya kushuhudia maonesho mbalimbali ya kitamaduni ikiwemo ngoma za asili, muziki wa tamaduni tofauti, maonesho ya sanaa na kazi za mikono, pamoja na warsha za kujifunza mila na desturi za mataifa mbalimbali. Aidha, kutakuwepo pia na maonesho ya vyakula vya asili na ufundi wa jadi kutoka maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa waandaaji, kongamano hilo limeandaliwa sambamba na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Utamaduni Duniani inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 21 Mei. Maadhimisho hayo yanasisitiza umuhimu wa kuhifadhi na kulinda utofauti wa tamaduni kama msingi wa maendeleo endelevu na kuishi kwa amani duniani.
Katika mchana wa kila siku ya mkutano, wageni watapata nafasi ya kutembelea maonesho ya utamaduni yatakayojumuisha mavazi ya jadi, sanaa za mikono, mapambo ya asili na vitu vya kihistoria kutoka nchi mbalimbali. Usiku kutakuwa na burudani za kitamaduni zitakazojumuisha muziki wa jadi, ngoma za asili na hadithi za kitamaduni kutoka mataifa tofauti.
Washiriki wa kongamano hilo wanatarajiwa kutoka katika taasisi za kimataifa, taasisi za ndani, vikundi vya sanaa na jamii mbalimbali. Watanzania na watu wa mataifa mbalimbali watakuwa wanufaika wakuu wa tukio hilo kwa kupata fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mahusiano ya kitamaduni.
Kwa upande wa ushiriki, waandaaji wameweka viwango mbalimbali vya udhamini na ushiriki ili kuruhusu wadau wengi kushiriki. Kundi la Gold Sponsor litatakiwa kuchangia shilingi milioni 15 na litapata nafasi kubwa ya kutambulika pamoja na kuandaa usiku maalumu wa utamaduni. Kundi la Grey Sponsor litachangia shilingi milioni 10, huku Silver Sponsor likiwa na ada ya shilingi milioni 2.5 kwa wizara, taasisi, wafanyabiashara na wajasuriamali wa kazi za sanaa na utamduni.
Kwa mujibu wa mpango wa bajeti uliotolewa, jumla ya shilingi milioni 221.3 zinatarajiwa kutumika katika maandalizi ya mkutano huo. Fedha hizo zitatumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo ukumbi wa tukio, usalama, usafiri, matangazo na utangazaji, miundombinu ya jukwaa, pamoja na burudani za vikundi vya utamaduni kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.
Tume ya Taifa ya Taifa ya UNESCO Tanzania ina jukumu la kuratibu shughuli za UNESCO nchini kwa mujibu wa sheria ya CAP.433 R.E 2023, ikihusisha serikali, mashirika ya kiraia na wadau wengine katika kulinda na kukuza utofauti wa tamaduni. Taasisi hiyo pia husaidia serikali katika kuandaa sera na mikakati ya kukuza sekta za utamaduni na ubunifu.
Waandaaji wanaamini kuwa kongamano hilo litasaidia kuongeza uelewa na kuthamini tamaduni mbalimbali, kuimarisha ushirikiano wa kitamaduni kati ya mataifa, pamoja na kutoa fursa kwa wasanii na vikundi vya sanaa kujitangaza kimataifa. Pia unatarajiwa kuchochea maendeleo ya sekta za ubunifu na kuacha msingi imara kwa miradi mingine ya utamaduni katika siku zijazo.
Kwa Mawasiliano zaidi kuhuu kongamano hilo piga simu namba 0754864257


Toa Maoni Yako:
0 comments: