Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Broadcasting Corporation (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha, amevunja ukimya na kujibu vikali wakosoaji wake, akisisitiza kuwa mafanikio hayatokani na kuwashambulia wengine bali juhudi binafsi, maono na nidhamu ya maisha.

Kupitia ujumbe wake, Dkt. Rioba alisema amekuwa akipokea maneno ya kejeli na dhihaka kutoka kwa baadhi ya watu wanaomuita “chawa” na kudai kuwa baada ya kuondoka madarakani atarejea kwenye maisha magumu.

Akielezea historia yake, alisema alizaliwa katika familia ya kawaida ya mwalimu wa shule ya msingi na kupitia changamoto nyingi za maisha, ikiwemo uhaba wa mahitaji muhimu katika utoto wake.

Aliongeza kuwa hakuwahi kuwa na mtu wa kumsaidia kupata nafasi za uongozi, bali alijituma katika elimu yake akasoma shule ya Ilboru na baadaye Makerere University, kabla ya kuwa mhadhiri katika University of Dar es Salaam.

Dkt. Rioba pia alibainisha kuwa aliwahi kupata fursa za kufanya kazi katika vyuo vikuu vya nje ya nchi, ikiwemo Kanada na Namibia, lakini alizikataa kwa hiari yake ili kuitumikia Tanzania.

Alisisitiza kuwa mafanikio hayawezi kupatikana kwa njia ya kulaumu, kutukana au kuwachafua wengine, bali kwa kuwa na maono, mikakati madhubuti, ubunifu na nidhamu katika utekelezaji wa malengo binafsi.

“Ndugu zangu, huwezi kufanikiwa kwa kuwavunjia heshima wengine. Mafanikio yanahitaji juhudi, nidhamu na mtazamo chanya wa maisha,” alieleza.

Aidha, alikosoa utamaduni wa baadhi ya watu kuishi kwa kulaumu na kukashifu wengine badala ya kujitafakari na kuchukua hatua za kuboresha maisha yao.

Katika ujumbe wake, Dkt. Rioba aligusia pia umuhimu wa mfumo wa elimu unaozingatia si tu kusoma, kuandika na kuhesabu, bali pia kufikiri na kubuni (K5), ili kujenga jamii yenye uwezo wa kujitegemea na kutatua changamoto zake.

Alimalizia kwa kueleza kuwa anatarajia kuanzisha safu maalum ya makala ambapo atajadili changamoto za kifikra na kijamii zinazoikumba Afrika, akilenga kuhamasisha mabadiliko ya mtazamo kwa maendeleo ya bara hilo.

Kauli hiyo imeibua mjadala mpana miongoni mwa wananchi, huku baadhi wakimuunga mkono na wengine kuendelea kukosoa msimamo wake.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: