Na Mwandishi Wetu.
Dar es Salaam — Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa adhabu mbalimbali kwa klabu na waamuzi kufuatia matukio ya kinidhamu yaliyojitokeza katika michezo ya Ligi Kuu ya NBC, ikiwemo kuifungia mchezaji wa Young Africans, Djigui Diarra, na kuipiga faini klabu ya Simba SC.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na TPLB, Diarra amefungiwa mechi tatu pamoja na kutozwa faini ya Sh milioni 2 baada ya kumshambulia mwamuzi kufuatia mchezo kati ya Mtibwa Sugar na Young Africans uliomalizika kwa sare ya 1-1 katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Aidha, mchezaji huyo pia ametozwa faini nyingine ya Sh milioni 2 kwa kosa la kuonesha ishara isiyo ya kiungwana kwa mwamuzi baada ya kumalizika kwa mchezo huo.
Katika hatua nyingine, klabu ya Simba SC imetozwa faini ya Sh milioni 10 baada ya mashabiki wake kuwarushia waamuzi chupa za maji walipokuwa wakitoka uwanjani kufuatia mchezo dhidi ya Pamba Jiji FC uliomalizika kwa sare ya 1-1. Tukio hilo limetajwa kuwa ni la kujirudia ndani ya kipindi kifupi.
Kwa upande wa klabu ya TRA United, nayo imetozwa faini ya Sh laki tano baada ya wachezaji wake kuonyeshwa kadi zaidi ya tano katika mchezo mmoja dhidi ya Young Africans, hali inayokiuka kanuni za nidhamu za ligi.
Sambamba na adhabu hizo, TPLB pia imewachukulia hatua baadhi ya waamuzi wa mechi husika. Mwamuzi wa kati, Gilbert Mrina, ameshushwa daraja kwa kushindwa kuchukua hatua stahiki kwa kosa la kinidhamu lililofanywa na mchezaji Diarra, huku mwamuzi msaidizi Abdulaziz Ally akifungiwa mechi tano kwa kushindwa kutafsiri vyema sheria ya mpira wa miguu katika tukio la kuotea.
TPLB imesisitiza kuwa hatua hizo zimechukuliwa kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu ili kuhakikisha nidhamu, haki na uwazi vinaendelea kudumishwa katika mashindano hayo.



Toa Maoni Yako:
0 comments: