Dar es Salaam — Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, ametembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambacho ni miongoni mwa taasisi kongwe na muhimu nchini, akieleza kuwa ni eneo lenye kumbukumbu kubwa kwake na lililomfungulia dunia katika safari yake ya elimu na maendeleo.

Katika ziara hiyo, Mhe. Ulega alipata fursa ya kumsalimia na kufanya mazungumzo ya kina na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Anangisye, ambapo walijadili kwa kina masuala ya maendeleo ya taifa hususan katika sekta ya ujenzi, uhandisi, pamoja na fursa zilizopo kwa wahandisi wazawa vijana.

Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Waziri Ulega alisema Profesa Anangisye alimkaribisha kushirikiana kwa karibu na chuo hicho kwa kutumia wataalamu waliopo, wakiwemo wakufunzi na wanafunzi, katika kutoa mapendekezo ya kitaalamu yatakayosaidia kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo zinazolikabili taifa.

Katika mwendelezo wa ziara yake, Mhe. Ulega alipata wasaa wa kuwasalimia walimu waliomfundisha masomo ya Microbiology, Aquatic Science na Chemistry, akiwemo Profesa Lymo, aliyekuwa mwalimu wake wa Microbiology, ambapo walipata fursa ya kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya nchi na mchango wa sayansi katika ustawi wa jamii.
Aidha, Waziri huyo alibainisha kuwa katika kuhakikisha serikali inarudisha mchango wake kwa jamii, Wizara ya Ujenzi itafanya marekebisho ya miundombinu katika baadhi ya barabara zilizopo ndani na maeneo ya jirani ya chuo hicho, hususan uwekaji wa taa za barabarani, hatua itakayosaidia kuboresha usalama, kuvutia mazingira ya chuo na kuendelea kukipa hadhi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama kitovu cha elimu nchini.

Mhe. Ulega alisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za elimu ya juu ili kuhakikisha ujuzi na rasilimali watu waliopo nchini vinatumika kikamilifu katika kuleta maendeleo endelevu ya Taifa.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: