Mtaalam kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mjiolojia Mbeleye David akizungumza na wateja wanaofika kuuza dhahabu zao.
Na Mwandishi Wetu, Singida.
Wadau wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji, wachenjuaji na wafanyabiashara wa madini mkoani Singida wamepongeza uwepo wa Soko la Madini Singida, wakisema limeleta mapinduzi makubwa katika biashara ya madini kwa kuimarisha uwazi, haki na ufanisi kupitia matumizi ya mfumo wa bei elekezi za kidigitali.
Akizungumza katika soko hilo, Mtaalam kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mjiolojia Mbeleye David, amesema kuanzishwa kwa soko hilo kumeleta tija kubwa kwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini kwa kuweka mifumo inayowalinda dhidi ya udanganyifu wa ubora wa dhahabu na unyonyaji wa bei.
Amesema kabla ya kuanzishwa kwa masoko ya madini, mkoa wa Singida ulikuwa unaratibu kiasi kidogo cha uzalishaji, kati ya gramu 100 hadi 200 pekee, lakini kwa sasa kupitia masoko hayo umefanikiwa kuratibu uzalishaji unaoanzia kilo 50 hadi 60 kwa wachimbaji wadogo, hali inayoonesha ongezeko la ufanisi na imani ya wadau katika mfumo huo.
David ameeleza kuwa Serikali imeweka mfumo madhubuti wa bei elekezi unaolenga kumlinda mchimbaji mdogo dhidi ya kupunjwa kwa kuuza madini kwa bei duni.
Amesema soko hilo limewekewa mashine ya kisasa ya X-Ray Fluorescence (XRF) kwa ajili ya kupima ubora wa dhahabu, hatua inayohakikisha madini yanauzwa kwa kuzingatia viwango sahihi vya ubora na thamani halisi.
Ameongeza kuwa, tofauti na awali ambapo bei elekezi ilitolewa kwa dhahabu ghafi pekee, kwa sasa soko linatumia ubao wa kidigitali unaoonesha bei elekezi za madini mbalimbali ikiwemo dhahabu, shaba na fedha, jambo lililoongeza uwazi na kuondoa mianya ya udanganyifu katika biashara ya madini.
“Teknolojia hii imeongeza uwazi na kurahisisha shughuli za masoko ikiwemo uthaminishaji wa madini na utoaji wa vibali vya kusafirisha madini ndani na nje ya nchi, ambazo sasa zinafanyika kwa wepesi na kwa haraka zaidi,” amesema David.
Kwa upande wake, mfanyabiashara wa madini, Abubakari Omary, amesema pamoja na mafanikio yaliyopo, elimu kuhusu matumizi ya bei elekezi inapaswa kuendelea kutolewa kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ili kuepusha sintofahamu na migogoro wakati wa kufanya biashara.
“Elimu ni msingi muhimu ili kila mdau aelewe haki na wajibu wake na kufanya biashara kwa kuzingatia bei halisi ya soko,” amesema Omary.
Aidha, wadau wamepongeza mfumo mpya wa masoko ya madini unaowawezesha wachimbaji wasio na leseni kujisajili na kuuza madini yao moja kwa moja katika masoko ya madini bila kulazimika kutumia leseni ya mfanyabiashara, hatua ambayo imeondoa kikwazo kikubwa kilichokuwepo awali.
Kwa ujumla, uwepo wa Soko la Madini Singida umetajwa kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya sekta ya madini mkoani humo, kwa kuongeza uwazi na usalama wa biashara, pamoja na kuongeza mapato ya serikali kupitia kudhibiti na kuzuia utoroshaji wa madini.
Mtaalam kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mjiolojia Mbeleye David, amesema kuanzishwa kwa soko hilo kumeleta tija kubwa kwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini kwa kuweka mifumo inayowalinda dhidi ya udanganyifu wa ubora wa dhahabu na unyonyaji wa bei.
Mfanyabiashara wa madini, Abubakari Omary, amesema pamoja na mafanikio yaliyopo, elimu kuhusu matumizi ya bei elekezi inapaswa kuendelea kutolewa kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ili kuepusha sintofahamu na migogoro wakati wa kufanya biashara.
Bi. Reticia Seni kutoka kampuni ya Dealer Ofisi ya Nganyila Lyapi Sweki, akihudumia wateja (hawapo pichani), waliokwenda kuuza dhahabu zao sokoni.Madini ya dhahabu yakipimwa kwenye mizani ya kielektroniki ili kujua uzito wake.




Toa Maoni Yako:
0 comments: