*Prof. Mkenda aisifu kama kinara wa udhamini, RC Babu ahimiza miundombinu

KILIMANJARO, Januari 3, 2025: Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umepongezwa kwa mchango wake mkubwa katika kuendeleza utalii ikolojia na michezo baada ya kuendelea kuwa mdau mkuu wa Tamasha la Rombo Marathon, tukio linaloimarisha kalenda ya michezo ya mwisho wa mwaka na kuvutia wadau mbalimbali wa riadha.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rombo, Prof. Adolf Mkenda, wakati wa tamasha hilo linalofanyika kila mwaka Desemba 23 katika Msitu wa Hifadhi wa Rongai.
Profesa Mkenda alisema TFS imekuwa kinara wa udhamini tangu kuanzishwa kwa marathon hiyo, hatua inayochangia mafanikio ya michezo na uhifadhi wa mazingira kwa wakati mmoja.
“Kwa namna ya pekee nawapongeza na kuwashukuru TFS kwa mchango wao mkubwa tangu tamasha hili lilipoanzishwa. Naomba pongezi hizi ziwafikie Kamishna wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo. Hongereni sana,” alisema Prof. Mkenda.
Mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, aliungana na pongezi hizo kwa kuipongeza TFS kwa kutumia michezo kama jukwaa la kukuza utalii ikolojia, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha miundombinu ya utalii ili kuongeza mvuto wa mashindano na vivutio vya asili.
“Nami nawapongeza. Endeleeni kuboresha miundombinu ya utalii ikolojia ili siku moja hata Kamati ya Ulinzi na Usalama iweze kufurahia kulala msituni,” alisema Mhe. Babu.
Kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TFS, Profesa Dos Santos Silayo, Naibu Kamishna wa Uhifadhi TFS, Emmanuel Wilfred, alisema wakala huo umejipanga kuendelea kuweka mazingira bora ya utalii ikolojia nchini, hususan kupitia ulinzi wa misitu, upandaji miti na ushirikiano na matukio ya michezo.
Rombo Marathon imefanyika kwa mara ya nne mfululizo tangu kuanzishwa kwake, ikiwa na lengo la kuwakutanisha wananchi wa Rombo na wadau wa michezo kama njia ya kukuza uhifadhi wa mazingira, kuimarisha undugu na kusherehekea msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Picha za Matukio mbalimbali ya ushiriki wa TFS kwenye Rombo Marathon, tarehe 23 Desemba 2025 ndani ya Shamba la miti Rongai, Rombo Tarakea - Kilimanjaro















Toa Maoni Yako:
0 comments: