Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM – Changamoto zinazowakabili watengeneza maudhui wa kidijitali zimewekwa mezani, baada ya Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, kukutana na watayarishaji 40 wa YouTube kutoka Chanika, jijini Dar es Salaam, na kuahidi kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na taasisi husika.
Katika kikao hicho kilichofanyika Jumamosi, Januari 24, 2025, watengeneza maudhui hao waliwasilisha kwa uwazi hoja zao, zikiwemo ukosefu wa mafunzo ya kitaalamu, changamoto za mitaji, mazingira ya kisheria yasiyoendana na kasi ya teknolojia, pamoja na uhaba wa masoko ya uhakika kwa kazi zao.
Watayarishaji hao wanaongoza vikundi mbalimbali vya sanaa vyenye zaidi ya wanatasnia 200 wanaojishughulisha na utengenezaji wa filamu na maudhui ya burudani ndani ya viunga vya Chanika, eneo linaloibuka kwa kasi kama kitovu kipya cha ubunifu wa kidijitali.
Akizungumza baada ya kusikiliza hoja hizo, Dkt. Kasiga alisema tasnia ya filamu na maudhui ya mtandaoni ni nguzo muhimu ya uchumi wa ubunifu, hivyo Serikali ina wajibu wa kuhakikisha inakua katika misingi imara ya kitaalamu na kisheria.
“Nimewasikiliza kwa makini. Hoja hizi zinahitaji ushirikiano mpana na taasisi mbalimbali, na nipo tayari kuratibu vikao hivyo ili mtapata majibu ya moja kwa moja,” alisema Dkt. Kasiga.
Aliwapongeza watengeneza maudhui hao kwa ubunifu wao na kwa mchango wao katika kutoa ajira kwa vijana, sambamba na kueneza ujumbe chanya kwa jamii kupitia kazi zao.
Aidha, aliwahimiza wanatasnia hao kujitokeza kujisajili na kujirasimisha chini ya Bodi ya Filamu Tanzania, akisisitiza kuwa hatua hiyo itawawezesha kunufaika na fursa mbalimbali zitakazotolewa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo ya tasnia.
Kikao hicho kimeibua matumaini mapya kwa watengeneza maudhui, wengi wao wakieleza kuwa hatua ya Serikali kusogea karibu na kusikiliza changamoto zao ni mwanzo wa mabadiliko chanya katika kukuza tasnia ya filamu na maudhui ya kidijitali nchini.










Toa Maoni Yako:
0 comments: