Na Mwandishi Wetu, Rabat – Morocco.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Paul Christian Makonda, amekutana na Rais wa Shirikisho la Kandanda Barani Afrika (CAF), Dkt. Patrice Motsepe, jijini Rabat, Morocco na kukabidhi rasmi barua maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika kikao hicho, Mhe. Makonda aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, amemhakikishia Dkt. Motsepe kuwa Rais Samia yupo tayari kushirikiana kwa karibu na CAF katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya mpira wa miguu barani Afrika, ikiwemo mashindano makubwa ya kimataifa.
Makonda amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika maandalizi ya kuwa mwenyeji wa Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuonesha tofauti kubwa katika ubora wa maandalizi na uendeshaji wa mashindano hayo ikilinganishwa na yaliyopita. 

Aidha, amemuomba Rais wa CAF kuiangalia Tanzania kwa jicho la kimkakati ili juhudi na uwekezaji unaofanywa na Serikali viweze kuzaa matunda makubwa yanayotarajiwa.

Kwa upande wake, Dkt. Motsepe amemshukuru Rais Samia kwa barua na salamu za ushirikiano, akieleza kuwa CAF inaithamini sana Tanzania na ipo tayari kufanya kazi bega kwa bega na Serikali kuhakikisha maendeleo ya kandanda yanafikiwa kwa kiwango kikubwa. 
Amesema amefurahishwa na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kukuza soka, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo, mafanikio ya maandalizi na uendeshaji wa mashindano ya CHAN 2024 pamoja na hatua mbalimbali zinazoendelea kuelekea AFCON 2027.

Motsepe pia ametangaza kuwa CAF itatuma timu ya wataalamu kwenda Tanzania kwa ajili ya kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa michezo katika kukamilisha maandalizi ya AFCON 2027, mashindano ambayo yanatarajiwa kushirikisha timu 28 badala ya 24. 

Ameongeza kuwa yupo tayari kuitembelea Tanzania hivi karibuni ili kujionea maendeleo ya maandalizi na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Serikali.
Hatua hiyo inaendelea kuipa Tanzania heshima kubwa kimataifa na kuthibitisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kutumia michezo, hususan soka, kama nyenzo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: